2017-01-14 12:48:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: kuna ukame na njaa!


Nchini Tanzania, Sekta ya Kilimo ni muhimili wa maendeleo ya uchumi. Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya 75% ya Watanzania. Kilimo kina uhusiano na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia uhusiano wa usafishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi na uuzaji nchi za nje; Inatoa malighafi kwa viwanda na soko kwa bidhaa zilizotengenezwa. Tanzania inazalisha takribani 97% ya mahitaji yake ya chakula. Uzalishaji wa mazao ya chakula unatofautiana mwaka hadi mwaka kutegemea kiasi cha mvua kilichopatikana.

Maendeleo ya kilimo yamekuwa chini ya Serikali/fedha za umma kwa kipindi kirefu. Hata hivyo marekebisho ya uchumi kwa jumla yamekuwa na yanaendelea kuwa na matokeo ya muhimu kwenye sekta ya kilimo. Marekebisho ya kiuchumi yamesababisha kufunguka sekta hiyo kwa uwekezaji binafsi katika uzalishaji na usindikaji, uagizaji pembejeo za kutoka nchi za nje na usambazaji na masoko ya kilimo. Serikali imebaki na kazi ya usimamizi na usaidizi wa umma na dhima ya uwezeshaji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuguswa na hali tete ya uhaba wa mvua katika shughuli za kilimo katika kipindi hiki ambacho kilipaswa kuwa ni kipindi cha mvua na kutokana na uhaba mkubwa wa chakula kwa baadhi ya maeneo, linawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali ili kumlilia Mwenyezi Mungu aweze kuwaletea mvua ya kutosha kwa ajili ya shughuli za kilimo. Haya yameandikwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza al Maaskofu Katoliki Tanzania katika barua yake iliyotiwa mkwaju hapo tarehe 13 Januari 2017.

Anasema, waamini wasali kwa ajili ya kuombea mvua nchini Tanzania ili Mwenyezi Mungu aliyewatunza wana wa Israeli walipokuwa safarini kuelekea kwenye Nchi ya Ahadi kwa kipindi cha miaka 40 awaangalie pie watanzania kwa wema, huruma na upole. Maaskofu wanawashauri waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwapatia baraka juu ya kazi za kilimo ili wapate mazao ya nchi, hatimaye waweze kumtumikia Mungu kwa moyo wenye utulivu na shukrani. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasema, ziadhimishwe Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea mvua, zifanywe hija, mafungo, mikesha na maombi maalum kwa ajili ya lengo hili, kwani aombaye hupewa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.