2017-01-13 10:13:00

Nigeria: Watu 800 wamefariki dunia na Makanisa 16 kuchomwa moto!


Mwenyeheri Paulo VI anasema, amani ni chachu ya maendeleo ya watu na kwamba: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni mabo yanayotishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii. Changamoto hii inaweza kupewa ufumbuzi wa pekee kwa kujikita katika utawala wa sheria, haki, usawa kati ya watu; upendo; ukweli na uhuru wa kweli unaothamini na kuheshimu mipaka ya watu husika! Hizi ni tunu msingi katika mchakato wa kukoleza na kudumisha amani duniani!

Migogoro ya wafugaji na wakulima Barani Afrika inapaswa kuvaliwa njuga, kwa kuwasaidia wahusika kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kushirikiana, kwani wote wanategemeana katika kukuza mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu! Katika kipindi cha miezi mitatu yaani kuanzia Mwezi Septemba hadi Desemba 2016 zaidi ya watu 800 wameuwawa kikatili na Makanisa 16 kuchomwa moto na Kikundi cha Kigaidi cha Fulani, huko Kusini mwa Nigeria anasema Askofu Joseph Danlami Bagobiri wa Jimbo Katoliki Kafanchan wakati alipokuwa anahojiana na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji hivi karibuni mjini Roma.

Amani, utulivu na mafungamano ya wananchi wa Nigeria yanatatizwa na uwepo wa makundi ya kigaidi nchini humo yanayoendelea kupandikiza hofu na kifo kwa watu wasiokuwa na hatia nchini humo. Kati ya mwezi Septemba 2016 hadi mwishoni mwa Mwaka 2016, Kikundi cha kigaidi cha Fulani, kilichoma moto vijiji 53, kikaunguza nyumba 1, 422 na kuchoma moto Makanisa 16. Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi mwaka 2014 takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya Wakristo 12, 000 waliuwawa kikatili na vikundi mbali mbali vya kigaidi nchini Nigeria, yaani Boko Haram na Fulani ambao kimsingi ni jamii ya wafugaji.

Kikundi cha Kigaidi cha Fulani kimekuwa ni chanzo kikuu cha mgogoro na wakulima Kusini mwa Nigeria. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, watu wanajichukulia sheria mikononi mwao na kudhani kwamba, sehemu nyingine ya jamii ni watu wa kuja na kupita! Biashara haramu ya silaha ambazo zimeangukia mikononi mwa Kikundi cha Kigaidi cha Fulani ni tishio kwa amani, usalama na mafungamano ya kijamii Kusini mwa Nigeria. Ikumbukwe kwamba, wakulima mna wafugaji wanategemeana na kukamilishana katika maisha yao, kumbe, hapa kuna haja ya kujenga utamaduni wa amani, haki na maridhiano, ili kukoleza kasi ya maendeleo ya watu: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.