2017-01-13 09:26:00

Jitoseni bila ya kujibakiza kwa ajili ya haki, amani na upendo!


Wapendwa Taifa la Mungu, leo tunaanza kipindi cha kawaida cha mwaka wa kanisa. Kipindi hiki hutanguliwa na maadhimisho ya mafumbo makuu ya Mungu kujifanya mwanadamu – kipindi cha Noeli. Mtakatifu Atanasi anasema Mungu amejifanya mtu ili mwanadamu awe Mungu. Noeli ni ufunuo wa juu kabisa wa Mungu. Ni upendo wake kwa wanadamu. Hapa mapenzi ya Mungu na upendo wake kwa wanadamu vyaonekana wazi – Tito 3:4…. Sisi tunaalikwa kuishi mapenzi hayo na upendo huo hapa duniani. Wajibu wetu ni kueneza mapendo na haki, kuachana na kila aina ya ubaya na uovu.

Wale wa kwanza waliopata habari ya kuzaliwa mwokozi, yaani wachungaji na wale wa kwanza waliofunga safari, yaani Mamajusi wanatuambia mengi sana juu ya ufunuo huo. Ni moyo mnyenyekevu tu unaoweza kutambua na kupokea mambo haya – utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema – Lk. 2:4. Sisi tunamshukuru Mungu aliyejifanya mtu ili tuweze kumwona – vinginevyo Mungu wetu angebaki mbali – wa kusikika sikika tu. Akajifanya mtu, akawa mtoto – ili sisi tumkaribie Mungu – chombo cha haki, amani na upatanisho.

Ndugu zangu, sasa tuko katika kipindi cha kawaida cha mwaka wa kanisa. Ni kipindi cha kuweka katika matendo kile ambacho tumesikia, kuona na kuelewa katika kipindi cha noeli. Sisi tunaamini katika historia inayojifunua na tunaamini katika ufunuo wa ukamilifu wa Mungu na wokovu wake. Ndiyo maana mtume Paulo anasema katika Ekaristi Takatifu tunasherehekea au tunaadhimisha kifo cha Bwana mpaka atakapokuja – 1 Kor. 11:26. Majilio yetu yako wazi katika kushiriki mapenzi haya ya Mungu. Sisi tumealikwa kushiriki katika ujenzi huu wa ufalme wa Mungu.

Katika maandiko inajulikana wazi kuwa fumbo ni tendo la upendo wa Mungu linalojifunua kadiri ya muda na wakati  kwa faida ya mwanadamu. Ukamilifu wa fumbo ulidhihirika katika ujio wake Kristo. Tunapoanza mwaka mpya wa kanisa hatuna budi kuwa wazi katika mtizamo wetu ili kuondoa hali ya zamani na kuweka hali mpya. Kama ilivyo dhamira yetu dominika hii ya leo ambapo tunahimizwa kuvaa utu mpya ili kuwa huru kutimiza mapenzi yake Mungu na kuwa sadaka kwa wengine.

Katika somo la kwanza tunasikia habari ya wimbo wa mtumishi mwaminifu. Huyu mtumishi hafahamiki ila sifa yake kuu ni kuwa anaishi kwa ajili ya wengine, ni mtumishi. Katika wimbo wa nne – Isa. 52:13 – 53:12 huyu anaelezwa kama mtumishi anayeteseka na anayekufa kwa ajili ya dhambi za wengine. Kanisa la mwanzo linamwona Yesu Kristo kama ndiye huyo mtumishi anayeteseka na kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Huyu mtumishi anakuwa sasa ni wokovu kwa mataifa yote.

Katika somo la Injili, Yohane anatushirikisha ufahamu wake juu ya Kristo. Huyu ndiye mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Yesu Kristo ni mteule wa Mungu. Ile dhana ya mtumishi katika somo la kwanza la leo inapata maana mpya kadiri Yohane anavyotufunulia. Kwa ufahamu huu na kwa mapenzi yake Mungu, tumepata mkombozi anayetuweka huru na dhambi zetu na kwa hilo twaweza kupendana.  Mtume Paulo katika Somo la pili anasema kuwa ufahamu huo kati yetu ndio unaotuwezesha kuongea juu ya  neema na amani na hutuwezesha kuendelea kukua katika fumbo la wokovu wa Mungu.

Tutumie mfano wa maisha ya Mtakatifu Maximillian Koble ili utusaidie pia kuelewa ujumbe wa neno la Mungu dominika hii ya leo. Mtakatifu Maximillian Maria Kolbe alitoa maisha yake kwa ajili ya wengine. Akiwa gerezani wakati wa utawala wa unazi huku akitambua nguvu ya uzima wa kimungu alijitolea kufa ili kumpatia nafasi yule mfungwa mwenzake kijana akiamini kuwa unazi utamalizika siku moja. Huyu Mtakatifu alitambua nguvu ya uzima na hivyo kifo hakikumtisha. Kwa ushuhuda huu anatualika tuvunje minyororo ya kifo inayoonekana katika maisha yetu, mazingira yetu, hali zetu n.k. Kwa maisha yake ya ushuhuda anadhihirisha wazi kuwa kwa kuzaliwa kwake Mwana wa Mungu, ufalme wa Mungu upo kati yetu. Hatuna budi pia sisi kudhihirisha kwa maisha yetu kwamba Mungu amezaliwa kati yetu na ndiye uzima wa milele. Kwa ushuhuda huu dhana ya mtumishi anayeteseka na anayetoa maisha yake kwa ajili ya wengine inanapata maana mpya.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.