2017-01-12 13:58:00

Mshikamano na wahamiaji kutoka Mexico na Amerika ya kati!


Kwa muda wa miaka 25, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB., limekuwa likiadhimisha Juma la Wakimbizi na Wahamiaji kama kielelezo cha mshikamano wa upendo na udugu na wananchi wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi kutoka Mexico na katika nchi za Amerika ya Kati. Maadhimisho ya Mwaka huu kuanzia tarehe 8- 14 Januari 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “kujenga utamaduni wa kukutana” ili kuwakutanisha wakimbizi na wahamiaji wa zamani na hawa wapya, ili kushirikishana matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Wakimbizi na wahamiaji ni chachu ya matumaini kwa watu walioacha yote nyuma yao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi nchini Marekani! Ni watu wanaokabiliana na changamoto na matatizo ya dhuluma, unyonywaji na ubaguzi wa kila aina! Historia ya maisha na changamoto za watu hawa zinaweza pia kupata mwangwi kwa watu wengi wa familia ya Mungu nchini Marekani, kwani hata wengi wao wanakumbushwa kwamba, kuna wakati walikuwa ni wakimbizi na wahamiaji, lakini sasa ni raia wa Marekani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linakaza kusema, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilionja pia adha ya kukimbilia kwenda nchini Misri, ili kutoa hifadhi na kuokoa maisha ya Mtoto Yesu aliyekuwa anatafutwa kwa kuuwawa kwa upanga wa Herode, Mfalme katili. Maadhimisho haya ni nyenzo muhimu sana katika mchakato wa kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutambua na kuthamini umuhimu wa wakimbizi na wahamiaji katika mchakato wa ustawi na maendeleo endelevu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linawakumbusha kwamba, kimsingi, familia ya Mungu nchini Marekani ina utamaduni na mapokeo ya kuwa ni wakarimu kwa wageni wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora nchini mwao. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanapokewa na kuthaminiwa, ili hatimaye, waweze kuingizwa katika mchakato wa mafungamano ya kijamii. Huu ni mwaliko wa kuondokana na woga, hofu na wasi wasi zisizo na msingi wala mashiko, tayari kujenga utamaduni wa maridhiano ya kijamii na kwamba, kwa njia ya neema ya Mwenyezi Mungu wanaweza kuvuka makwazo haya ambayo wakati mwingine, yamehatarisha sana amana ya ukarimu, mshikamano, upendo na udugu kati ya raia wa Marekani na wakimbizi pamoja na wahamiaji.

Umoja na mshikamano wa kidugu ni nyenzo muhimu katika maisha ya watu. Kuna haja kwa Serikali ya Marekani kuendeleza sera na mikakati ya kuwapokea na kuahudumia wakimbizi na wahamiaji, kwani kwa njia ya ukarimu na upendo, kuna watu waliweza kuwahudumia Malaika pasi ya wao kufahamu! Hivi ndivyo Kardinali Daniel N. DiNardo pamoja na Askofu mkuu Josè Horacio Gòmez, Rais na Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu katoliki Marekani wanavyoandika katika ujumbe wao wa maadhimisho ya Juma la Wakimbizi na Wahamiaji nchini Marekani kwa Mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.