2017-01-11 13:41:00

Waluteri Duniani kwa Mwaka 2017: Upendo na mshikamano!


Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani anasema, mwaka 2017 umetengwa maalum kwa ajili ya kukuza na kudumisha upendo, mshikamano na haki kati ya watu wa mataifa. Haya yamo kwenye ujumbe wake wa Mwaka Mpya kwa Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani yapatayo 145. Amewakumbusha kwamba, wokovu unapatikana kwa njia ya imani, kumbe, wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, wanashuhudia na kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Huu ni ulimwengu ambao unaendelea kuchechemea kwa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kumbe, hapa kuna haja kwa Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo, haki na mshikamano wa dhati; chachu ya mabadiliko ya wema na huruma ya Mungu kwa walimwengu. Mwenyezi Mungu amewaahidia watu wake kwamba, atawapatia moyo wa nyama na kuwaondolea moyo wa jiwe kama kielelezo cha huruma na upendo wake kwa binadamu. Mwenyezi Mungu anayafanya yote haya si kwa mastahili ya binadamu bali ni kwa njia ya neema ya Mungu ambayo ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Dr. Martin Junge anakaza kusema,  neema ya Kristo inaendelea kulisha na kurutubisha maisha ya waamini, ili kwa njia yao pamoja nao, Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri, sehemu mbali mbali za dunia yaweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya neema ya Mungu inayoyachachua malimwengu. Kuanzia tarehe 10- 16 Mei 2017, Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani litafanya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Mambo makuu yanayopewa kipaumbele cha kwanza ni: Umuhimu wa Mageuzi ya Kiluteri Duniani, changamoto ya kuendelea kuyatolea ushuhuda katika maisha na utume wa Makanisa mahalia.

Jambo la pili, ni Uwajibikaji wa Kiekumene, unaopania pamoja na mambo mengine kuendelea kuimarisha mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani na Kanisa Katoliki, kama ilivyoshuhudiwa hivi karibuni kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, sanjari na makubaliano katika kukuza na kudumisha upatanisho ndani ya familia ya Makanisa ya Kiluteri Duniani.

Jambo la tatu, kwa waamini wa Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani ni kutambua kwamba, mchakato wa Mageuzi ya Kiluteri Duniani, hata kama imekwisha gota miaka 500, bado kabisa yanaendelea katika maisha na utume wa Kanisa, ili kutambua na kuendeleza utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu duniani; wokovu ambao ni neema ya Mungu kwa waja wake. Hii ni changamoto endelevu ya kusikiliza kwa makini ujumbe wa wokovu na kuumwilisha katika matendo ya huruma na upendo; kwa kuwa na moyo wa nyama, unaoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani. Dr. Martin Junge anahitimisha ujumbe wake kwa Mwaka Mpya wa 2017 kwa kusema, kwa njia ya kutangaza, kushuhudia na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani yanaweza kuwa kweli ni chachu ya upendo, mshikamano na haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.