2017-01-11 09:07:00

Kanisa nchini Poland linataka kuwekeza kwa utume wa vijana!


Enendeni mkaitangaze Injili, ni kiini cha ujumbe mkuu wa mpango mkakati wa kichungaji kwa Kanisa nchini Poland kwa mwaka 2016-2017. mwaka huo wa kichungaji nchini humo, waamini hasa vijana, watauishi kwa imani, wongofu wa ndani, ubatizo na kwa utangazaji wa Injili, kumshuhudia Kristo katika maisha ya kila siku. Askofu mkuu Stanislaw Gadecki, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, na Askofu mkuu wa Poznan, amefafanua kwamba wamependa kuzama katika matatizo na matunda yanayotokana na umoja wao ndani ya Kristo, umoja ulioanza kwa safari ya ubatizo. Kila mbatizwa anaitwa kuitangaza Injili ya Kristo kwa maneno na kwa matendo. Katika Kanisa, kunahitaji kubwa la kuwashirikisha vijana na vipaji vyao katika shughuli za kichungaji, anasema Askofu mkuu Stanislaw Gadecki.

Ikumbukwe kuwa, Kanisa nchini Poland, lilikuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya vijana kimataifa mwaka huu 2016. Baada ya jubilee ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, Kanisa nchini Poland limeazimia kuadhimisha mwaka wa kitaifa kwa kumbukumbu ya Br. Albert, aliyefahamika kama Adam Hilary Bernard Chmielowski, mwanzilishi wa Shirika la watawa wa kiume la Mt. Francisko, mtumishi wa maskini. Shirika ambalo alilianzisha mwaka 1888, na baadae mwaka 1891 kuanzisha Shirika la masista ambalo alilikabidhi kwa Sr. Bernardyan Jablonska.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.