2017-01-11 11:35:00

Gambia dumisheni amani na umoja wa kitaifa ili kuokoa maisha!


Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Senegal linaitaka familia ya Mungu nchini Gambia kuonesha uvumilivu, utulivu na amani ili kuweza kukabiliana na machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza nchini humo baada ya Rais Yahya Jammeh kushindwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Gambia hapo tarehe 1 Desemba 2016. Rais Jammeh amekataa kata kata kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu kinyume kabisa na utashi wa wananchi na kwamba, Umoja wa Mataifa umethibitisha kwamba, uchaguzi ulikuwa ni halali na kwamba, Rais Adama Barrow aliyechaguliwa kidemokrasia anapaswa kushika madaraka kwa mujibu wa katiba ya Gambia hapo tarehe 19 Januari 2017.

Rais Jammeh amewaonjesha cha mtema kuni Mabalozi 12 waliomtaka kuachia ngazi badala ya kung’ang’ania madarakani kwa ajili ya ustawi na mafao ya wananchi wa Gambia ambao kwa sasa wako hatarini kutumbukia katika hali ya hatari zaidi. Askofu Paul Abel Mamba wa Jimbo Katoliki Ziguinchor, nchini Senegal kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Senegal ameitaka familia ya Mungu nchini Gambia kumaliza machafuko haya ya kisiasa kwa njia ya amani ili kuepuka umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Pande zote zinazohusika zinapaswa kupokea na kuambata amani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kukuzwa na kudumishwa kwa ajili ya mafao ya wengi! Hiki kiwe ni kipindi cha kushikamana zaidi ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu! Kupotea kwa amani nchini Gambia kutasababisha pia athari kwa nchi jirani kama Senegal ndiyo maana Baraza la Maaskofu Senegal linaendelea kuhimiza umuhimu wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ya kitaifa nchini Gambia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.