2017-01-10 12:13:00

Tanzania kuendeleza ushirikiano na China kwenye viwanda!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano na Serikali ya China katika nyanja mbalimbali kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu. Ametoa kauli hiyo Jumatatu, Januari 9, 2017 alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mheshimiwa Wang Yi, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema ushirikiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria, hivyo ameihakikishia Serikali ya China kwamba utaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa Mataifa yote mawili. Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini China kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini zikiwemo za miundombinu, viwanda, kilimo na nishati. “Tanzania iko tayari kupokea kampuni zaidi za China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini.Tupo tayari kupokea viwanda kati ya 200 hadi 700 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” amesema.

Kwa upande wake Mheshimiwa Wang Yi amepongeza utendaji kazi wa Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli pamoja na viongozi wengine hususan katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na tayari matunda yameanza kuoneka. “Serikali ya China kwa sasa iko katitka mkakati wa kuhamishia viwanda vyake vingi Barani Afrika. Iliamua kuichagua Tanzania kuwa moja katika ya nchi watakayohamishia viwanda hivyo kutokana na kuridhishwa na dhamira inayoonyeshwa na Serikali katika kuleta maendeleo,” amesema. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa China katika ziara hii Barani Afrika anatembelea pia DRC, Nigeria, Madagscar na Zambia.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.