2017-01-10 10:36:00

Askofu Nkwande: Dhambi ya ubinafsi ni chanzo cha kinzani!


Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kwa mwaka 2017 anasema, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni changamoto inayopaswa kutekelezwa na wadau mbali mbali na kwamba hii ni dhamana nyeti inayotakiwa kulindwa na kudumishwa; kwa kuzingatia: utu, heshima, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na haki msingi za binadamu. Vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kupandikiza mbegu ya hofu na kifo ni kielelezo cha umaskini wa maisha ya kiroho na kimwili.

Amani ya kweli inafumbatwa katika misingi ya mshikamano, upendo na ushirikiano wa dhati katika kupambana na changamoto zinazosababisha kutoweka kwa misingi ya amani duniani! Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda anasema, ilikudumisha misingi ya amani duniani kuna haja ya watu kutendeana haki mintarafu “Kanuni ya Dhahabu”, yaani upende kumtendea jirani yako, kile ambacho wewe ungependa hutendewe! Anasema, kuna mambo kadhaa ambayo yamekuwa ni chanzo kikuu cha kutoweka kwa amani duniani!

Baadhi ya mambo haya anasema, Askofu Kwande ni utumwa mamboleo unaowatumbukiza wasichana na wanawake katika biashara ya ngono; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake; nyanyaso na mauaji ya kikatili dhidi ya wazee na vikongwe; nyanyaso na dhuluma kwa watoto wadogo; rushwa na ufisadi sanjari na biashara ya silaha duniani inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Msingi wa mambo yote haya ni dhambi ya ubinafsi, uchu wa mali na madaraka bila kujali haki msingi za binadamu, utu, heshima, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Askofu Renatus L. Nkwande anakaza kusema, matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Lakini ikumbukwe kwamba, iko siku watu hawa wanaonyonywa na kukandamizwa watasimama na kudai haki zao msingi na hapo ndipo kutakapokuwepo na “patashika nguo kuchanika” kutokana na mapambano ya matabaka! Ili kukuza na kudumisha amani duniani kuna haja ya kujifunza kutenda na kuwafunda watu katika misingi ya haki kuanzia katika familia, Kanisa dogo la nyumbani, ili kweli haki iweze kurithishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Jambo la msingi anasema Askofu Nkwande, watu wenyewe wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki na kwa njia hii  haki na amani vinaweza kujengwa na kudumishwa na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.