2017-01-09 11:50:00

Hotuba ya Papa Francisko kwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Vatican


Usalama na amani ndiyo tema kuu iliyopembuliwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican wapatao 182 wakati wa kutakiana heri na baraka kwa Mwaka mpya 2017. Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na nchi mbali mbali duniani umeendelea kuimarika kwa viongozi wakuu kutembelea na kukutana na Baba Mtakatifu  na kwa namna ya pekee, wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliohitimishwa hivi karibuni. Kumekuwepo na makubaliano kati ya Vatican na nchi mbali mbali katika uhusiani kati ya Kanisa na Serikali, katika masuala ya fedha, kodi na siasa.

Baba Mtakatifu anasema, Vita kuu ya kwanza ya Dunia iliyofumuka kunako mwaka 1917 ilisababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na matokeo yake ni kuibuka kwa tawala za mabavu zilizopelekea mipasuko ya kijamii. Lakini, katika kipindi cha miaka 100 iliyopita amani na utulivu imekuwa ni chachu ya maendeleo, lakini kwa bahati mbaya haipewi kipaumbele cha kwanza. Hadi leo hii kuna mamilioni ya watu wanaoishi katika vita, kinzani na mispasuko ya kijamii.

Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inapaswa kuwa ni dira na mwongozo kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kujikita katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Dini mbali mbali duniani zinapaswa kuwa ni vyombo vya kukoleza na kuimarisha amani na usalama duniani. Dini zisaidie kuganga na kuponya majeraha ya chuki na kinzani za kihistoria, tayari kuanza mchakato wa kutembea pamoja kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi; kwa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli, uwazi, ushuhuda pamoja na sadaka inayotolewa na Mashuhuda wa imani kwa njia ya ya elimu; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi na huduma kwa waathirika wa vita na mipasuko ya kijamii.

Baba Mtakatifu anasema, hizi ni nyenzo zinazoweza kusaidia kukuza na kudumisha amani na usalama, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Kwa bahati mbaya, misimamo mikali ya kidini na kiimani inayofumbatwa katika vitendo vya kigaidi, imekuwa ni sababu ya maafa makubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kudiriki kutumia watoto wadogo katika mauaji kama ilivyojitokeza nchini Nigeria. Walengwa ni watu wanaosali, wafanyakazi, watalii au watu waanaofurahia maisha. Mauaji ya kigaidi ni kashfa kubwa kwani yanatumia jina la Mungu kupandikiza mbegu na utamaduni wa kifo; kimsingi anasema Baba Mtakatifu hakuna mauaji yanayopaswa kutendwa kwa jina la Mungu. Vitendo vya kigaidi ni matokeo ya umaskini wa maisha ya kiroho unaosababishwa pia na umaskini wa kijamii. Umaskini huu unaweza kuondolewa kwa njia ya ushirikiano kati ya viongozi wa kidini na kisiasa; kwa kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho zinazojikita katika hofu ya Mungu na upendo kwa jirani.

Kwa kutambua na kuthamini uhuru wa kidini na mchango wa dini katika ustawi na maendeleo ya jamii husika; kwa kuheshimu zawadi ya uhai pamoja na kusimama kidete, kupambana na umaskini; kwa kuthamini na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama mahali pa malezi, makuzi na ukomavu wa utu na heshima ya binadamu. Kumbe, anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika elimu na utamaduni; kwa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kupambana na tabia ya kupandikiza misimamo mikali ya kidini na kiimani; mambo yanayopelekea kushamiri kwa vitendo vya kigaidi duniani.

Elimu makini inaweza kusaidia kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii, amani na utulivu! Viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwasaidia wananchi wao kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya amani na usalama. Amani ni fadhila inayowahusisha wadau mbali mbali katika jamii. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema ndiyo maana amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku kwa kuheshimu: mafao ya binadamu, utu, heshima na haki zake msingi.

Ili kujenga msingi wa amani anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kupambana na vitendo vyote vinavyosababisha ukosefu wa haki, kwani haki na amani ni chanda na pete na inakamilishwa zaidi na msamaha unaoganga na kuponya majeraha ya mahusiano ya kibinadamu yaliyoharibiwa na ubinafsi. Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa waliopokea mwaliko wake wa kutoa msamaha kwa wafungwa kama kielelezo cha huruma inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwani huruma ni tunu msingi ya maisha ya kijamii.

Kwa hakika jamii nzima inaweza kujikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa huruma kwa kuguswa na mahangaiko ya wengine; kwa kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Haki zao msingi zilindwe, ziheshimiwe na wasaidiwe kuingizwa katika mafungamano ya kijamii ili kuwa na uhakika wa usalama pamoja na utambulisho wao wa kitamaduni na kisiasa. Wakimbizi na wahamiaji wanayo dhamana ya kuheshimu na kuzingatia sheria, tamaduni na mapokeo ya nchi inayowapatia hifadhi. Viongozi wa Serikali husika wanapaswa kuwa na sera na mikakati ya muda mrefu ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji bila kuathiri huduma za kijamii zinazopaswa kutolewa kwa wananchi wao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wakimbizi ni watu wenye majina, historia na familia. Hakuna amani ya kweli ikiwa kama binadamu hawataheshimiwa na kuthaminiwa badala ya kuangaliwa tu kwa takwimu za kiuchumi! Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake kwa kuwekeza katika ustawi na maendeleo ya watu, kwani maendeleo ni jina jipya la amani. Baba Mtakatifu anazipongeza: Italia, Ujerumani, Ugiriki na Uswiss kwa kuwa mstari wa mbele kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji ambao daima wameacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wake. Anawapongeza watu wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Anasikitika kusema, kwamba, hata katika mazingira haya kuna watu wanaothubutu kufanya biashara haramu ya binadamu kwa kuendelea kuwatumbukiza watu katika dimbwi la utumwa mamboleo. Ukosefu wa usawa, mwelekeo tenge wa maisha na utu wa mwanadamu; rushwa na ufisadi ni mambo yanayohatarisha amani na usalama wa watu na mali zao.

Kanisa katika Mwaka 2017 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapicha Waraka wa kitume “Populorum progression” yaani “Maendeleo ya watu” aliyekaza kusema: amani ya kweli inafumbatwa katika maendeleo ya watu; kwa kuwa na ugawanyaji sawa wa raslimali ya dunia; kwa kutengeza fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kusimama kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato; kwa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ili kuondokana na baa la njaa na utapiamlo unaotishia maisha ya watoto wengi duniani pamoja na kujenga utamaduni wa kuhifadhi chakula.

Watoto na vijana ni matumaini ya taifa la leo na kesho, kumbe, wanapaswa kuheshimiwana kuthaminiwa na kamwe wasinyanyaswe na kudhulumiwa utakatifu wa maisha kwa kupelekwa mstari wa mbele kama chambo wakati wa vita; kwa kufanyishwa kazi za suluba au kutumbukizwa katika biashara ya ngono, magenge ya kiuhalifu na wafanyabiashara wa utamaduni wa kifo! Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba mgogoro wa vita nchini Siria unapata suluhu ya kudumu; kwa kuzingatia sheria za kimataifa; ulinzi, usalama na huduma kwa raia.

Ili makubaliano ya kusitisha vita nchini Siria yaweze kutekelezwa kuna haja ya kupiga rufuku biashara ya silaha inayotishia amani sehemu mbali mbali za dunia kama ilivyo huko Korea ya Kaskazini. Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na upigaji rufuku wa kutengeneza, kuhifadhi na kutumia silaha ya kinyuklia. Vatican kwa upande wake, itaendelea kujikita katika kuhamasisha kanuni maadili ya amani na usalama ili kweli Mkutano wa Kimataifa kuhusu Silaha uweze kufanyika katika mazingira ya ukweli na uwazi pasi na hofu au tabia ya watu kujifungia katika ubinafsi wao.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika mshikamano, majadiliano na ushirikiano na kwamba, diplomasia ni chombo madhubuti katika kufanikisha mchakato wa amani duniani. Kanisa litaendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha upatanisho na matokeo yake ni uhusiano mpya kati ya Cuba na Marekani na mchakato unaoendelea huko nchini Colombia na Venezuela ambayo kwa sasa imetumbukia katika mpasuko wa kisiasa, kijamii na kiuchumi. Vatican inahimiza majadiliano ya kisiasa kati ya Israeli na Palestina pamoja na suluhu ya amani huko Mashariki ya Kati, DRC na Myanmar.

Vatican inaunga mkono mchakato wa kuviunganisha Visiwa vya Cyprus pamoja na kuendeleza mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ingawa inatambua kwamba, kuna majanga asilia ambayo pia yameendelea kusababisha maafa makubwa huko:  Equador, Italia na Indonesia. Ujasiri na mshikamano viwe ni nguzo msingi ya kuanza ujenzi wa maeneo yaliyoathirika na majanga asilia. Vatican inawashukuru viongozi wa Italia waliosaidia kuhakikisha kwamba kuna kuwepo ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa kusema, amani ni zawadi, changamano na dhamana inayopaswa kushughulikiwa na wote ili kuitafuta na kuidumisha. Amani ya kweli inafumbatwa katika utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wote amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.