2017-01-05 16:03:00

Iweni ni mashuhuda wa Injili ya miito kwa vijana!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kila mwaka, linaandaa kongamano la maisha ya kitawa na kazi za kitume, ili kushirikishana furaha ya maisha ya udugu na uzuri wa kuwa na mifumo mbali mbali ya miito kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni changamoto ya kuanza kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa Mwaka 2018 itakayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Lengo ni kuwasaidia vijana kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama chemchemi ya maisha iliyofichika chini ya ardhi lakini inabubujikia usafi na upya wa maisha.

Vijana wa kizazi kipya wanahitaji chemchemi ya maji safi itakayozima kiu ya safari ya tafiti na hamu ya kuwa na maisha bora zaidi. Vijana kwa kukutana na Kristo Yesu na kumwachia nafasi ya kuwashika mkono na kuwaongoza katika upendo wake, unawasaidia vijana kupata na kupanua wigo wa matumaini yasiyodanganya kamwe! Huu ndio mwelekeo wa huduma na mtindo wa kutangaza na kusindikiza miito mbali mbali. Hii ni dhamana inayohitaji ari na moyo wa majitoleo yanayomgusa mtu mzima anayetakiwa kulinda na kutunza njia ya maisha kama kasha linalotunza hazina inayopaswa kulindwa.

Hii ni sehemu ya hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Alhamisi tarehe 5 Januari 2017 kwa watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume waliokuwa wanashiriki katika kongamano la kitaifa la maisha ya kitawa na kazi za kitume lililoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Majitoleo na sadaka ya huduma na utume ndani ya Kanisa yanahitaji nidhamu kwa wale wanaowaongoza katika safari ya maisha ya kitawa, ili kutafuta kwa pamoja ile furaha ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa imani na matumaini, kinyume kabisa cha maisha ya vijana wengi wa kizazi kipya waliokosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi pamoja na hekima ya maisha. Lakini, ikumbukwe kwamba, hii ndiyo Saa ya Mungu!

Baba Mtakatifu anawataka watawa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza kwa makini vijana, kupoteza muda pamoja nao; kupokea maswali na kiu ya maisha yao. Kumbe, ushuhuda wa watawa unapaswa kuwa ni wenye mvuto unaosimikwa katika furaha na ukweli; kwa kusimulia uzuri, hali ya kushangwa na maajabu ya kupendwa na Mungu wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wengine ili hatimaye, kuacha chapa ya kudumu katika historia, changamoto inayohitaji watawa kujiaminisha kwenye huruma na upendo wa Mungu kwa kuishi kiaminifu maamuzi waliyofanya katika upya wa ule upendo wa kwanza!

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwa kusema, utangazaji wa miito si ufanisi wa mtu kwa kile anachokifanya bali ni matunda ya umakini na mang’amuzi ya kina; kwa kuangalia kwa mwelekeo chanya matukio mbali mbali ya maisha ya mwanadamu: wanayokutana nayo: kiroho na kimwili. Moyo ulioshangazwa na kuwa na shukrani kwa karama na mapaji waliyokirimiwa katika maisha; kwa kuonesha uwezo na mapungufu yake ya kibinadamu yaliyopo kwa sasa, yale yatakayokuja na kuendelezwa baadaye.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuwa na sera na mikakati yenye mwelekeo mpana zaidi katika shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito; mikakati inayofumbatwa katika umoja ili kusoma kwa ujasiri hali halisi kama ilivyo hata katika magumu na kinzani kwa kutambua alama ya ukarimu na wema wa moyo wa binadamu. Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, utamaduni wa miito unarejeshwa tena katika Jumuiya za Kikristo, ili kuwapatia vijana wa kizazi kipya ari na moyo wa kuwa na ndoto kubwa katika maisha; kwa kushangaa kunakowapatia nafasi ya kufurahia uzuri na hatimaye kuchagua tunu iliyoko ndani mwake, kwani inayapamba na kuyafanya maisha kuwa kweli!

Baba Mtakatifu anawataka watawa daima kutambua kwamba, wao ni utume na wala si kwamba, wako katika utume; wajifahamu kwamba wao ni sehemu ya utume wenyewe unaopaswa kushuhudia mwanga, kubariki, kuhuisha, kufufua, kuponya na kuokoa. Ni mwaliko wa kuwa na ujasiri wa kusema “Simama ondoka, usiogope! Hii pia ndiyo iliyokuwa kauli mbiu ya kongamano hili lililowashirikisha watawa zaidi ya 800 kutoka sehemu mbali mbali za Italia. Ni kauli mbiu inayowasaidia kufanya kumbukumbu ya historia ya maisha na wito wao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wengine, ili kutekeleza utume ambao Mwenyezi Mungu amewakabidhi kwa kutambua kwamba, yuko pamoja nao daima, kumbe, hawana sababu ya kuogopa! Anatambua udhaifu na mapungufu yao, anawasimamisha na kuwaimarisha siku kwa siku kwani ana uvumilivu usiokuwa na mipaka.

Roho Mtakatifu awaongoze ili waweze kuwa na ujasiri wa kutambua njia mpya za kutangaza Injili ya miito; kwa kuwa watu wenye ujasiri wa kupokea mwanga angavu wa mapambazuko; mang’amuzi mapya ya imani, ari na upendo kwa Kanisa na kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Roho Mtakatifu anawasukuma kuwa ni watu wenye uvumilivu wenye upendo usiotishika na kinzani zinazoibuliwa na moyo wa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.