2017-01-01 11:59:00

Papa Francisko asikitishwa na shambulio la kigaidi Uturuki!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe Mosi, Januari 2017 amewatakia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema heri na baraka za Mwaka mpya 2017 na kwamba, huu utakuwa ni mwaka mzuri, ikiwa kama kila mtu ataweza kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa msaada wa Mungu pamoja na kutenda mema kila siku! Kwa njia hii, watu wataweza kujenga na kudumisha amani duniani, kwa kukataa kishawishi cha kukumbatia: vita, chuki na uhasama; bali kwa njia ya maneno na matendo kushuhudia udugu na upatanisho.

Kanisa linaadhimisha Siku ya 50 ya Kuombea Amani Duniani iliyoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI, ili kuimarisha dhamana ya pamoja katika ujenzi wa amani na udugu duniani. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2017 ni “kutotumia nguvu: mtindo wa siasa ya amani”. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba hata wakati huu wa kutakiana heri, baraka na matumaini kwa Mwaka Mpya, kuna shambulizi ambalo limetokea huko Instanbul, nchini Uturuki, Jumamosi, usiku na kusababisha watu zaidi ya 39 kufariki dunia!

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wa karibu kwa wote wanaoguswa na kutikiswa na janga hili kwa kuondokewa na ndugu, jamaa na rafiki zao; anawaombea majeruhi ili waweze kupona haraka na kwamba, anapenda kuonesha mshikamano na familia ya Mungu nchini Uturuki.

Baba Mtakatifu Francisko, ametumia nafasi hii kumshukuru Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa salam na matashi mema wakati alipokuwa anatoa salam za Mwaka Mpya 2017 kwa wananchi wa Italia. Anawaombea wananchi wa Italia, ili kwa njia ya mchango wa uwajibikaji na mshikamano wa pamoja, wananchi wote waweze kuangalia ya mbeleni kwa imani na matumaini. Amewatakia heri na baraka wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kukuza na kudumisha amani duniani. Amewakumbuka kwa namna ya pekee watu wote walioshiriki katika maandamano ya amani yaliyoandaliwa na Jimbo kuu la Bologna! Amewatakia heri na baraka wanajumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa ushuhuda wao sehemu mbali mbali za dunia. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote heri, baraka na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu kwa Mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.