2016-12-30 10:05:00

Mchakato wa ujenzi wa diplomasia ya tunu msingi za kijamii!


Shirikisho la Wamissionari wa Upendo Kisiasa linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka ishirini tangu kuanzishwa kwake. Tangu wakati huo, limekuwa ni rejea makini katika majadiliano na upatanisho wa kimataifa, ili kukuza na kudumisha diplomasia inayofumbatwa katika tunu msingi za maisha. Shirikisho hili limeanzisha kozi mpya kwa ajili ya kuwafunda Mabalozi na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na Mashirika yao ya Kimataifa mjini Vatican. Mafunzo haya yanapania pamoja na mambo mengine, kusaidia kukoleza mchakato wa haki na amani jamii katika nchi husika pamoja na kudumisha mahusiano mema na nchi nyingine.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ujumbe wake kwa Shirikisho la Wamissionari wa Upendo Kisiasa anapenda kuwahimiza kuendeleza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. “Domus Carità Politica” anasema Kardinali Parolin, lina dhamana ya kuwaunganisha Mabalozi na wanadiplomasia wanaotekeleza dhamana na utume wao mjini Vatican, ili kukoleza ari na moyo wa ushirikiano; majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi mintarafu masuala tete na changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ni majadiliano pia yanayowahusisha viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican.

Katika mazingira kama haya kumeibuliwa taasisi ya Shirikisho la Upendo wa Kisiasa, inayojihusisha na utoaji wa semina mintarafu diplomasia ya tunu msingi za kijamii na kwa namna ya pekee kabisa: dini na diplomasia, ili kutengeneza mazingira yatakayosaidia kujenga na kudumisha nadharia inayotafsiriwa katika matendo. Lengo ni kuimarisha misingi ya haki, amani na maridhiano katika Jumuiya ya Kimataifa. Dini zina dhamana na mchango mkubwa katika kuimarisha mafungamano ya kijamii na kwamba, siasa inapaswa kukoleza amani jamii!

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, katika maadhimisho haya anasema, diplomasia ya Vatican inajipambanua kwa kuwa ni chombo cha huduma kwa binadamu; kwa kuhamasisha familia ya Mungu duniani kujikita katika kutafuta, kulinda na kudumisha mafao ya wengi; haki, amani, upatanisho na mafungamano ya kijamii, mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili!

Shirikisho la Upendo wa Kisiasa limetumia nafasi hii kufanya upembuzi yakinifu kuhusu masuala ya kijamii na kiuchumi; vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; mashambulizi ya kigaidi na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Limeangalia pia changamoto za ujenzi na uimarishaji wa Umoja wa Ulaya; hatari ya kutoweka kwa misingi ya haki na amani kimataifa, bila kusahau changamoto ya baa la njaa na umaskini duniani pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kanuni maadili upendo; kwa kujenga utamaduni wa majadiliano unaosimikwa katika huruma, kama alivyokazia Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Katika kipindi cha miaka ishirini, Shirikisho hili limeimarisha mafungamano ya kidiplomasia; urafiki na hali ya kuaminiana mambo msingi yanayokuza na kudumisha majadiliano yenye tija na mashiko kwa familia ya binadamu. Haya ni mazingira yanayosaidia kudumisha amani, ushirikiano na mafungamano ya kijamii kati ya watu wa mataifa na tamaduni mbali mbali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.