2016-12-30 10:47:00

Injili ya familia!


Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ni mahali pa kufundana umuhimu wa kumwilisha: huduma, upendo, ukarimu, msamaha na kuvumiliana. Hapa ni madhabahu ya sala, ibada, na tafakari ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayowawezesha wanafamilia kujivika upendo, busara, rehema, utu wema, upole na unyenyekevu.

Tunu hizi msingi za maisha ya ndoa na familia kwa sasa ziko hatarini kutokana na taasisi ya familia kupigwa vita kana kwamba ni “Mbwa koko!! Lakini, Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia! Tarehe 30 Desemba 2016, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kardinali Carlos Osoro Sierra, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania anaialika familia ya Mungu nchini Hispania kujizatiti katika ujenzi wa tunu msingi za familia kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa upendo, msamaha na maridhiano; mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia.

Waamini hawana budi kusimama kidete katika misingi ya imani, maadili na utu wema sanjari na kukataa kishawishi cha utengano na kinzani katika maisha ya ndoa na familia kwani waathirika wakuu ni watoto. Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” uwe ni dira na mwongozo katika utume na maisha ya familia ya Kikristo hatua kwa hatua. Kanisa litaendelea kuwa na jicho la kichungaji kwa ajili kuzisaidia familia za Kikristo kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake katika malezi na makuzi ya watoto wao pamoja na kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia katika mwanga wa Injili na utu wema!

Kardinali Carlos Osoro anasema, familia ya Kikristo ni mradi wa pekee katika ulimwengu mamboleo kwani inatoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Familia ya Kikristo inasimikwa katika Sakramenti ya Ndoa; muungano imara kati ya bwana na bibi, alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu, ambao Kristo Yesu, ameukabidhi kwa Kanisa lake kuumwilisha katika maisha na utume wake. Agano la ndoa linajikita katika upendo usiogawanyika na endelevu; malezi na makuzi ya watoto; umoja na udugu kama chachu ya ujenzi wa jamii inayojikita katika udugu, upendo na mshikamano.

Kardinali Carlos Osoro anahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kwa kukazia kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, upendo kati ya wanandoa unakua na kuendelea kuimarika, kwa kutambua changamoto, matatizo na fursa zinazoweza pia kujitokeza katika uhalisia wa maisha. Kutokana na kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kuna haja kwa wanandoa kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia umuhimu wa ndoa na familia katika ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili! Huu ni mwaliko wa kuiga mfano bora wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.