2016-12-28 11:25:00

Ujumbe wa Noeli kutoka kwa Familia ya Mungu Barani Afrika!


Kilio cha familia ya Mungu Barani Afrika wakati huu wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli ni haki, amani, upendo, mshikamano, umoja wa kitaifa, majadiliano ya kidini na kiekumene; ukweli katika upendo sanjari na kuondokana na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vitendo vya utoaji mimba, kifo laini na adhabu ya kifo; mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha Injili ya uhai, ambayo Mama Kanisa anaiadhimisha kwa namna ya pekee wakati huu wa Kipindi cha Noeli!

Kardinali Jean Pierre Kutwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abijan, nchini Pwani ya Pembe, ameitaka familia ya Mungu nchini humo kujikita katika Injili ya upendo, haki na amani kwa kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi; ili kujichimbia katika hija ya upatanisho, msamaha na umoja wa Kitaifa. Familia ya Mungu nchini Pwani ya Pembe inahamasishwa kuondokana na usiku na matendo ya giza na badala yake waanzishe mchakato wa upatanisho katika kweli na haki!

Kardinali Maurice Piat, Askofu wa Jimbo Katoliki la Port-Louis kwa kushirikiana na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani nchini Mauritius Askofu Ian Ernest, kwa pamoja wametia mkwaju katika Waraka wa Kiekumene unaowataka Wakristo kujisadaka bila ya kujibakiza ili kudumisha Uekumene wa huduma kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema anasema Askofu mkuu Denis Amuzu-Dzakpah wa Jimbo kuu la Lomè, nchini Togo kushikamana katika umoja ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na usalama kati ya watu!

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, nchini DRC ambako kunaendelea kuwaka moto wa hali tete ya kisiasa anasema, Familia ya Mungu nchini DRC inahamasishwa kuwa ni shuhuda na chombo cha ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano katika ukweli na uwazi. Machafuko ya kisiasa ni matokeo ya kumalizika kwa uongozi wa Rais Joseph Kabila, aliyeingia madarakani kunako mwaka 2001 na kipindi chake cha uongozi kikatiba kumalizika tarehe 20 Desemba 2016, lakini kutokana na makubaliano ya kisiasa ataendelea kuwepo madarakani hadi pale Rais mpya atakapochaguliwa.

Kardinali Pasinya anasema, Fumbo la Umwilisho ni changamoto ya kujikita katika misingi ya haki, amani,  msamaha, upatanisho na umoja wa kitaifa kwa kukataa kishawishi cha chuki, hasira, uhasama na vita! Amani ya kweli inajikita katika: ukweli, haki, upendo na uhuru; mambo msingi yanayoweza kuiepusha DRC kujikuta inaendelea kuzama katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Hiki ni kipindi kwa familia ya Mungu nchini DRC kuwa ni wajenzi wa haki, amani na upatanisho.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Benjamin Ndiaye wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal, anapinga kwa nguvu zote kwa Senegal kutaka kurudisha tena adhabu ya kifo iliyofutwa nchini humo kunako mwaka 2004 kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu! Amelaani vitendo vya unyanyasaji, dhuluma na kipigo cha wanawake majumbani na kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuzama katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kanuni maadili na utu wema, ili kweli familia iweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani; shule ya haki, amani, upendo na ukarimu. Amani inayoletwa kwa kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, itawale akili na mioyo ya watu, kwa kuishuhidia kwa njia ya Furaha ya Injili katika kipindi hiki cha Noeli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.