2016-12-28 08:27:00

Mwongozo wa mahubiri makini!


Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa anasema kwamba, Mwongozo wa Mahubiri uliotolewa na Baraza lake hivi karibuni una pania pamona na mambo mengine kufafanua umuhimu wa mahubiri katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kwamba, mahubiri yanapaswa kuandaliwa kikamilifu kwa kujikita katika Neno la Mungu na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa.

Hii ni sanaa ambayo Wakleri wanapaswa kujifunza na kuiendeleza katika mahubiri yao na kwamba, mahubiri si jambo la mchezo, kwani linahitaji maandalizi maalum, ili kweli Neno la Mungu liweze kuwagusa watu kutoka katika undani wa maisha yao ya kiroho. Mwongozo huu una pania kuwa ni chombo cha kuwasaidia Wakleri kutekeleza dhamana na utume huu nyeti katika maisha na utume wa Kanisa, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Furaha ya Injili, Evengelii gaudium.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walionesha umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa, kwa ajili ya kumpatia Mwenyezi Mungu, utukufu na mwanadamu kutakatifuzwa, kwa kuwashirikisha Watu wa Mungu katika ukamilifu wake. Neno la Mungu linapaswa kutangazwa na kufafanuliwa wakati wa Liturujia ya Neno katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kweli Neno hili liweze kuwa ni chachu ya mabadiliko kwa Mhubiri na mwamini anayesikiliza mahubiri haya.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mahubiri wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhimu sana kwani hapa ni kilele cha majadiliano kati ya Mungu na mwanadamu, kabla ya mwamini kushiriki Mkate wa uzima, chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Mahubiri wa kati wa Ibada ya Misa takatifu yana umuhimu wa pekee kabisa, tofauti na Katekesi inayoweza kutolewa nje ya Ibada ya Misa takatifu.

Wakleri, yaani Maaskofu, Mapadre na Mashemasi wanakumbushwa kwamba, mahubiri ni sehemu muhimu sana ya mafundisho yao kwa familia ya Mungu, changamoto ya kujiandaa kikamilifu, kwa kutambua kwamba, wanatangaza Habari Njema ya Wokovu kwa niaba ya Yesu Kristo mwenyewe, kwa kuwasaidia waamini kung’amua utajiri wa Neno la Mungu kutoka katika undani wa mioyo yao, ili Neno hili liweze kuwaletea mabadiliko yanayokusudiwa. Mahubiri yaliyotolewa na Mababa wa Kanisa kama vile Mtakatifu Ambrosi, Mtakatifu Agostino, Mtakatifu Leo mkuu ni kielelezo muhimu sana cha Mafundisho yao msingi kwa familia ya Mungu waliyokuwa imekabidhiwa kwao na Mama Kanisa.

Mashemasi nao wanachangamotishwa na Mama kanisa kuhakikisha kwamba, wanajiandaa barabara kuwahubiria Watu wa Mungu, Neno lenye utajiri na mang’amuzi makubwa katika maisha, kumbe wanapaswa kujiandaa barabara bila kufanya mzaha. Mahubiri si jambo la kushtukiza, linahitaji maandalizi ya kutosha, kwa kutambua lengo la Kanisa kwa ajili ya watoto wake, kwa kuangalia Kanisa linafundisha nini kutoka katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu na kwa ajili ya tukio maalum, ili kuweza kuzima kiu ya maisha ya kiroho inayojionesha kwa waamini wanaokusanyika kwa ajili yak usali.

Mahubiri anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Injili ya Fuaraha,  yanapaswa kuwa ni matunda yanayobubujika kutokana na tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Sala pamoja na kusoma alama za nyakati kwa ajili ya mahitaji ya shughuli za kichungaji katika eneo husika. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji Sakramenti ya Upendo, Sacramentum caritas anasema, mahubiri yaliyoandaliwa barabara ni msaada mkubwa katika majiundo endelevu ya dhamiri nyofu miongoni mwa waamini.

Mahubiri yanahabarisha na kumuunda mwamini kutoka katika undani wa moyo wake, kuhusu kile ambacho Mama Kanisa anakiri na kuungama, yaani Kanuni ya Imani, kile ambacho Kanisa linaadhimisha, yaani Sakramenti za Kanisa, kile ambacho Mama Kanisa anahimiza waamini kukiishi, yaani Amri kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu na mwishowe, kile ambacho Kanisa linamwilisha kwa njia ya imani tendaji, yaani maisha ya sala! Wahusika wakuu wa Mwongozo huu, anasema Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa ni Mapadre, Mashemasi na Majandokasisi. Huu unaweza kuwa ni msaada mkubwa kwa wadau mbali mbali wanaojihusisha na majiundo awali na endelevu kwa Wakleri. Mwongozo huu, uwe ni msaada mkubwa katika kuhamasisha tafakari, usikivu na umwilishaji wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.