2016-12-28 09:23:00

Kilio cha Watoto Mashahidi waliofutiliwa mbali kwa upanga wa Herode


Mama Kanisa tarehe 28 Desemba ya kila Mwaka anaadhimisha Sherehe ya Watoto Mashahidi waliomshuhudia Kristo Yesu si kwa maneno bali kwa kuyamimina maisha yao kutokana na ukatili wa Mfalme Herode. Watoto hawa wanalikumbusha Kanisa kwamba, kifo dini ni zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake. Hawa ni watoto waliouwawa kikatili kwa upanga wa Mfalme Herode aliposikia kwamba, kuna Mfalme amezaliwa mjini Bethlehemu. Hivi ndivyo walivyofanya pia kwa Mtakatifu Stefano Shahidi na Mwinjili Yohane; matukio ambayo yanakumbukwa kwa namna ya pekee na Mama Kanisa wakati huu wa Kipindi cha Noeli. Siku kuu hii ilianza kuadhimishwa na Kanisa kunako karne ya VI kadiri ya taarifa za Kitabu cha Orodha ya Majina na Habari za Wafia dini cha Yerome!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli kwa mwaka 2016 amewakumbuka kwa namna ya pekee, watoto wanaoendelea kufutiliwa mbali na upanga wa Herode kutokana na vita, baa la njaa, magonjwa, ukatili, nyanyaso na majanga asilia; pamoja na ubinafsi unaofanywa na watu wazima. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajizatiti ili kulinda utakatifu wa maisha, utu, heshima na haki msingi za watoto. Lengo ni kuwawezesha watoto kufurahia malezi, makuzi na utoto wao pasi na kubebeshwa mtutu wa bunduki kwenda mstari wa mbele badala ya kucheza na kufurahia maisha na watoto wenzao au kutumbukizwa katika biashara haramu ya dawa za kulevya, viungo vya binadamu na utumwa mamboleo. Mambo yote haya ni ukatili dhidi ya ubinadamu!

Shirika la Kimissionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam,  kila mwaka linaadhimisha kumbu kumbu ya Watoto Mashahidi kama siku yao maalum, inayowakusanya watoto kutoka katika Parokia zote za Jimbo kuu la Dar es Salaam, ili kumzunguka Kardinali Polycarp Pengo, aweze kuwatia shime na ari ya kuwa ni Wamissionari kati ya watoto wenzao wanaoteseka na kusumbuka kutokana na sababu mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.