2016-12-27 08:18:00

Simameni kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya familia!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini limepokea kwa mikono miwili, Wosia wa Kitume uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” na kuwaalika wanafamilia ya Mungu kuwapokea, kuwasaidia na kuwasindikiza wanandoa wanaoogelea katika dimbwi la shida na mahangaiko katika maisha ya ndoa na familia, ili kuwaonjesha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Maaskofu wanasema, huruma na upendo ni kiini cha Wosia wa Baba Mtakatifu kuhusu maisha ya ndoa na familia, kwani ukweli na uwazi kwa Roho Mtakatifu hauna haja ya sheria wala maelekezo ya kibinadamu! Waamini wanapaswa kuonesha moyo wa upendo, huruma na mshikamano kwa wanafamilia wanaojitahidi kurejea tena Kanisani ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa baada ya kutembea gizani kutokana na hali yao ya maisha ya ndoa na familia.

Waamini kamwe wasimezwe na malimwengu kwa taarifa zinazotolewa na magazeti pamoja na vyombo vya habari vinavyotaka kuuza habari za udaku kwa kupindisha ukweli, kwani Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia mintarafu Mafundisho tanzu ya Kanisa kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika shughuli za kichungaji zinazofanywa katika utume wa familia ndani ya Kanisa!

Maaskofu wanasema, Baba Mtakatifu yuko makini katika Wosia wake wa kitume unaojikita kwanza kabisa katika: Neno la Mungu,Mapokeo ya Kanisa, Kanuni ya Imani, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Wosia huu umeandikwa na Baba Mtakatifu huku akiwa na jicho la kichungaji, ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa katika maisha ya ndoa na familia kwenye ulimwengu mamboleo.

Kwa bahati mbaya, familia ni kati ya taasisi ambazo zinashambuliwa kwa kiasi kikubwa katika ulimwengu wa maendeleo ya utandawazi na sayansi na tekknolojia. Kutokana na ukweli huu, utume wa ndoa na familia ni changamoto kubwa katika Kanisa. Kumbe, kuna haja kwa Kanisa, kuanzia kwenye kitovu cha familia kufanya kazi kwa pamoja ili kweli familia ya Kikristo iwe ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, haki na amani; mahali pa kujifunza kutoa na kupokea huruma inayojikita katika huduma makini ya upendo.

Hii ni changamoto inayogusa familia nzima ya Mungu nchini Ufilippini, yaani: Wakleri, Watawa na Waamini walei katika ujumla wao! Katika maisha na utume wa Kanisa, asiwepo mtu anayetengwa na badala yake, waamini wawe ni chachu, vyombo na mashuhuda wa mageuzi yanayojikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Familia zisimame kidete kutangaza, kutetea na kushuhudia Injili ya familia kwa watu wa mataifa sanjari na kuendelea kuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa sala, tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha ushuhuda wa imani tendaji. Kila mwamini anayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba anajenga na upendo na udumifu wa maisha ya ndoa na familia wanasema Maaskofu kutoka Ufilippini katika Barua yao ya kichungaji wanapoendelea kutafakari kwa kina na mapana kuhusu Wosia wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.