2016-12-27 07:57:00

Maneno ya ushuhuda wa Kinabii kutoka kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko ni mtu asiyependa maneno mengi bali matendo yanayomwilishwa katika maisha ya watu kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji na sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwasha moto wa mawasiliano katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kwani kuna kitabu ambacho kimeandikwa na kinaanza kuuzwa madukani “Misamihati ya Papa Francisko”. Haya maneno ya ushuhuda wa kinabii katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ni maneno 50 ambayo yamechaguliwa kwa uangalifu mkubwa na wataalam wa mawasiliano ya jamii kutoka ndani na nje ya Vatican. Utangulizi wa kitabu hiki, umeandikwa na Askofu Nunzio Galantino, katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Misamihati ya Baba Mtakatifu ni maneno ambayo yanatumiwa na Papa Francisko walau katika maisha na utume wake, kielelezo cha mwendelezo wa mambo makuu katika maisha yake ili kusaidia mchakato wa kuboresha ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Haya ni maneno yanayogusa undani wa mtu na kumtaka afanye maamuzi, alete mageuzi ili hatimaye aweze kuwa ni mtu mwema zaidi kwake na kwa jirani wanaomzunguka!

Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican katika tafakari yake juu ya uzinduzi wa kitabu hiki anasema, Baba Mtakatifu Francisko ni mtu wa upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu si haba kabisa kwamba, wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu alijiwekea utaratibu wa kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya matendo ya huruma. Ni Baba wa kazi na wala si wa “kupiga ngebe”! Wengine wangethubutu kusema, hapa ni kazi tu hadi kieleweke!

Maneno 50 ni ushuhuda unaofumbatwa katika maisha yake ya kila siku yaliyopembuliwa na waandishi wa habari pamoja na wataalam wa mawasiliano ili kuelezea utajiri wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni mwaliko wa kumwangalia Baba Mtakatifu katika mapana ya maisha na utume wake, ili kugundua chemchemi ya huruma na upendo inayobubujika kutoka kwake anapokutana na watu, ili kuwashirikisha furaha, huruma na upendo wa Kristo na Kanisa lake.

Waandishi wa habari na wataalam wa mawasiliano walioshiriki kuandika kitabu hiki ni wale ambao kutokana na taaluma na wajibu wao wa kila siku wanajikuta wako bega kwa bega na Baba Mtakatifu Francisko na matokeo yake ni kazi hii nzito na pevu inayochangia mchakato wa kuona utajiri wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha ya watu: kiroho na kimwili. Dr. Greg Burke anakaza kusema, misamihati hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumjifunza Baba Mtakatifu Francisko, tayari kushiriki pamoja naye katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu duniani kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Msamihati wa maneno 50 ya Baba Mtakatifu Francisko ni chachu ya maboresho ya dunia, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi anasema Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.