Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, ni wakati mwingine tena wa kuendelea kutafakari kiundani, ule ujumbe wa Barua ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko, ijulikanayo kama “Misericordia et misera”, yaani Huruma na amani. Katika barua hii, Baba Mtakatifu anatuasa kwamba, kusikiliza Neno la Mungu ni kitu muhimu sana katika maisha ya mkristo na mwanadamu kwa ujumla. Anatuambia kila Jumapili Neno la Mungu linatangazwa kwa kila Jumuiya ya wakristo ili Siku ya Bwana ipate kuangaziwa na mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!
Katika adhimisho la Ekaristi Takatifu, anendelea kutuambia Baba Mtakatifu, ndiyo sehemu muhimu ambapo tunashuhudia mahaojiana ya ndani baina ya mkristo na Mungu, yaani mahojiano ya kiliturujia na hapa mkristo, hupata kuingia ndani katika kutafakari Neno la Mungu na kuisikia sauti ya Mungu inenayo ndani yake na hivyo, kutuwezesha kutafakari zaidi safari yetu ya wokovu, katika kutangaza kazi ya huruma ya Mungu isiyokuwa na mwisho.
Mungu anendelea kuongea nasi leo hii kama rafiki, na hasa katika Maandiko Matakatifu ili tu apate kutusindikiza katika safari ya maisha. Na ni katika Maandiko Matakatifu, tunaona na kujifunza matendo makuu ya Mungu yahusuyo huruma, na hivyo kila mmoja wetu anapata kushiriki upendo wa kimungu toka mwanzo wa Uumbaji, na hii ndiyo alama ya upendo wa Mungu kwa ulimwengu. Kupitia maneno ya Manabii na Maandiko ya Hekima, Roho Mtakatifu anafanya upya historia ya Wana wa Israeli kama alama ya kutambua Huruma ya Mungu na ukaribu wa Mungu kwa mwanadamu, ingawa mara nyingi mwanamu huyu amekuwa ni mdhambi na hata kutokuwa mwaminifu katika njia ya kumcha Mungu.
Hivyo, hakika ujio wa Kristo na mafundisho yake, umeanzisha historia mpya katika Jumuiya ya mwanadamu. Katika ujio huu wa Kristo tunatambua maana ya juu kabisa ya Huruma ya Mungu na msamaha, na hii inatuletea amani nafsini mwetu kwani, kupitia kwa Kristo tunapanishwa na Mungu na kuwa wana wa Mungu. Kupitia Maandiko Matakatifu ambayo daima yamewekwa hai katika Kanisa, Kristo anaendelea kuongea na Kanisa na hivyo kuendelea kuliwezesha Kanisa kufikisha Injili kwa kila kiumbe. Injili hii ndiyo Habari Njema, habari iletayo matumaini, habari iletayo wokovu na habari iletayo amani nafasi mwetu. Katika kusikiliza Habari Njema yaani Injili, hasa kila Jumapili ambapo pia ni jukumu la kila mkristo, tunapata utajiri wa neema za Huruma ya Mungu nafsini mwetu, na kuendelea kutufanya tuwe na hamu ya kusonga mbele na kutaka kutafakari kila wakati Maandiko Matakatifu, Anasema Baba Mtakatifu.
Hivyo ndugu yangu, barua hii ya kitume ya Baba Mtakatifu, ifufue upya ndani mwetu hamu ya kupenda kusoma, kusikiliza na kutafakari tena zaidi na zaidi Neno la Mungu ili kupata kufanywa wapya katika Bwana. Nakutakia heri na baraka katika kuzidi kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Kwa namna ya pekee, kabisa Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuandaa vyema mahubiri yao ili kutangaza Ukweli na Uzuri wa Injili unaowafunuliwa waamini huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mahubiri na Katekesi ambayo kimsingi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala inapaswa daima kuchota utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu.
Kutoka katika studio za Radio Vatican ni mimi, Padre, Agapiti Amani, ALCP/OSS.
All the contents on this site are copyrighted ©. |