2016-12-26 11:21:00

Ujumbe wa Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa Noeli 2016


Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha Noeli anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa kina Fumbo la Umwilisho, yaani kuzaliwa kwa Yesu Kristo anayewakirimia walimwengu amani, inayopaswa kumwilisha matumaini kwa njia ya ushuhuda wa haki, upendo na maridhiano kati ya watu! Yesu Kristo ni kielelezo cha mwanga wa matumaini, furaha, amani na maana ya maisha ya kweli! Fumbo la Umwilisho iwe ni nafasi ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za watoto wanaoendelea kuteseka kutokana na sababu mbali mbali duniani!

Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli wamekazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa watanzania  kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuendelea kujikita katika kanuni maadili na utu wema ili kuondokana na matendo ya giza yanayofumbatwa katika rushwa, ufisadi na utendaji wa kazi unaofanywa kwa mazoea! Kipindi cha Majilio kilikuwa ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya waja wake!

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salam amewataka watanzania kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa mshikamano wa upendo na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kila mtanzania anahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya nafasi yake. Amewataka watanzania wote kuwa ni vyombo, mashuhuda na chemchemi ya haki, amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Kwa upande wake Askofu Augustine Ndeliakyama Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar, anasema, watanzania wanaonesha Imani yao kwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli pamoja na Rais Mohamed Shein ambao wanaendelea kujizatiti katika kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi; kwa kukazia kanuni maadili, utu wema na uwajibikaji kwa watanzania wote ili kuliwezesha taifa “kuchanja mbuga” katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Askofu Shao anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya watanzania wasiokuwa na nia njema kwa mafao, ustawi na maendeleo ya wengi, wanaotaka kukwamisha mchakato wa mabadiliko yanayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano! Amewataka viongozi kuendelea kukaza kamba ili kweli mageuzi yanayosimamiwa kwa sasa yaweze kuwanufaisha watanzania wengi. Jambo la msingi kwa Serikali ni kujikita katika utawala wa sheria, haki msingi za binadamu; haki na amani na uwajibikaji pasi na ubaguzi! Watanzania wenye mapenzi mema wataendelea kuwaunga mkono hadi kieleweke!

Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida katika mahubiri yake pamoja na mambo mengine amekazia kwa namna ya pekee dhamana na wajibu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowaathiri watu wengi. Kuna uhaba mkubwa wa mvua nchi Tanzania kutokana na uharibifu wa mazingira. Matukio mbali mbali ya maisha iwe ni fursa ya kupanda mti na kuboresha mazingira kama mwendelezo wa kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitekeleza!

Askofu Telesphory Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro amekazia nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na kiasi ili kuondokana na matabaka yaliyokuwa yanaanza kujengeka nchini Tanzania kwa kuwa na matajiri wa kutupwa na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Kuna haja kwa serikali na watu binafsi kubana matumizi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi katika maisha ya watu!

Askofu Severin NiweMugizi amewataka watanzania kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu ili kuondokana na vitendo na maisha ya dhambi na giza kwa kutambua uwepo wa Mungu kati yao; Mungu anayekuja kuwakomboa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Waamini wawe tayari kumpokea na kumkaribisha Yesu ili aweze kuzaliwa tena katika maisha yao, licha ya ugumu na ukata wa maisha; wasi wasi na hofu ya kutumbuliwa wakati wowote; kuyumba kwa biashara na pato la watu wa kawaida pamoja athari za watumishi hewa!

Askofu NiweMugizi katika mahubiri yake wakati wa mkesha wa Noeli anasikitika kusema kwamba, baadhi ya Hospitali zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa zitalazimika kupunguza wafanyakazi wake kutokana na ukata baada ya kubainika kwamba kulikuwepo pia wafanyakazi hewa katika taasisi hizi! Jambo hili ni nyeti sana linahitaji majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya afya ya wanzania wa kawaida, vinginevyo, watu wengi watakimbilia kwa waganga wa jadi au kujikatia tamaa huko huko vijijini kwani wengi wao hawana bima ya afya! Kuna watu walioathirika kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, hao nao bado wanaendelea kusubiri msaada wa hali na mali ili kuanza tena upya, baada ya kuwapoteza ndugu na jamaa pamoja na makazi yao.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, sasa watanzania wote bila ubaguzi wanaisoma namba! Kumekuwepo na kimya kikuu katika vyama vya kisiasa nchini Tanzania! Wengine wanasema, kuna ”mnyauko wa kisiasa”, lakini bado kuna mapambano kati ya jamii za wakulima na wafugaji, mambo yanayohatarisha amani na mafungamano ya kijamii! Bado kuna ukatili wa kijinsia na nyanyaso dhidi ya watoto wadogo; yote haya ni matendo ya giza yanayopaswa kuondolewa kati ya watanzania.

Askofu Severine NiweMugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara ameichambua hali ya maisha ya watanzania kama karanga na kusema, hata katika Makanisa mambo si shwari sana kwani waamini wanakimbilia kwenye Makanisa yanayoahidi miujiza ya njia za mkato katika maisha! Fedha za chapuchapu pasi na kufanya kazi! Upwonywaji wa magonjwa na ibada zenye midundo na kwamba, Ibada zinazojikita katika Heri Nane za Mlimani ambazo ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu, eti hizo zimepitwa na wakati! Kumbe, Fumbo la Umwilisho, yaani kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, iwe ni fursa kwa waamini kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha nao na kwamba, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kutembea katika mwanga wa maisha mapya, imani na matumaini pasi na kukata wala kukatishwa tamaa!

Rais John Pombe Magufuli katika salam na matashi mema kwa watanzania wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Katoliki Singida amewataka watanzania kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuchapa kazi kwa nguvu, juhudi na maarifa, ili kweli Tanzania iweze kuwa ni nchi ya viwanda. Rais Magufuli pia amekemea udini, ukabila, itikadi na ukanda usiokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watanzania wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Kwa msaada wa vyombo vya mawasiliano Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.