2016-12-24 15:06:00

Lindeni na kudumisha utakatifu wa maisha ya watoto na haki zao msingi


Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linaathiri kwa kiasi kubwa haki msingi za watoto, kiasi kwamba wengi wao wanajikuta wakikabiliwa na magonjwa na kifo katika umri mdogo. Vita, kinzani na migogoro ya kijamii na kisiasa inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia imekuwa na madhara makubwa kwa maisha,  malezi na ukuaji wa watoto kiroho na kimwili, kiasi hata cha kuwapoka matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaendelea pia kusababisha madhara makubwa kwa watoto katika maisha yao, kwani wanajikuta kwamba wanatumbukizwa katika ulimwengu wa ulaji wa kupindukia. Jumuiya ya Kimataifa imeutangaza Mwaka 2017 kuwa ni Mwaka wa Utakatifu wa Maisha ya Watoto. Watu wote wanahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki; ukuaji na malezi endelevu ya ya watoto wadogo.

Hiki ndicho kiini cha Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2016 unaotolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho yamemwezesha Neno wa Mungu, Yesu Kristo kufanyika mwili na kukaa kati pamoja na watu wake, changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kudumisha utakatifu wa maisha ya watoto duniani. Kwa bahati mbaya Injili ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu inaendelea hata leo hii kutangazwa na kushuhudiwa katika maeneo yenye vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, matokeo yake ni maafa na majanga makubwa katika utu na heshima ya binadamu; ukosefu wa usawa na haki jamii. Watoto sehemu mbali mbali za dunia wanajikuta wakiwa wamezungukwa na madhara ya vita, dhuluma, nyanyaso, ubaguzi, magonjwa, njaa na umaskini wa kutupwa. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakumbusha kwamba, tarehe 16 Aprili 2016 akiwa ameandamana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Askofu mkuu Jerome wa Jimbo kuu la Athens, walitembelea Kisiwa cha Lesbos, Ugiriki ili kujionea wenyewe mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji, hasa watoto waliokuwa wanateseka kutoka na ubaguzi wa rangi na kidini na dhuluma mbali mbali zinazoendelea kuongezeka kila kukicha!

Inasikitisha kuona kwamba, hata watoto wanaoishi katika Nchi zilizoendelea zaidi duniani nao pia wanakabiliwa na umaskini wa maadili na utu wema kutokana na kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; mateso na nyanyaso za aina mbali mbali. Ni watoto ambao wanaathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii, hususan matumizi makubwa ya televisheni na mitandao ya kijamii ambayo inapatikana hata katika simu za viganjani. Maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano yamechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika mfumo wa mawasiliano ya kijamii, kiasi cha kuwageuza watoto hawa kuwa ni walaji wa kupindukia wa bidhaa zinazozaliwa viwandani katika soko la vifaa vya umeme. Maendeleo haya yanaathari kubwa sana katika ukuaji na maendeleo ya watoto: kiroho na kimwili!

Kwa upande wake, Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2016 inayoadhimishwa nchini Russia hapo tarehe 7 Januari 2017 anasikitika kusema Mapinduzi ya Mwaka 1917, yapata miaka mia moja iliyopita yameleta mageuzi makubwa ya  maisha ya wananchi wengi wa Russia kwa kuwatumbukiza katika vita ya wenyewe kwa wenyewe! Mapinduzi haya yamepelekea kuporomoka kwa miundo mbinu ya Serikali na huo ukawa ni mwanzo wa madhulumu na nyanyaso za kidini nchini Russia, kiasi cha kuacha mpasuko mkubwa wa kijamii nchini humo.

Changamoto kwa sasa ni kuanzisha mchakato wa mafungamano ya kijamii, kidini na kisiasa ili kujenga umoja wa kitaifa nchini Russia. Madhulumu na nyanyaso za kidini zinaendelea kuzalisha makundi makubwa ya mashuhuda wa imani nchini Russia. Damu ya mashuhuda hawa wa imani itakuwa ni chemchemi ya ujenzi wa Russia mpya katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Patriaki Cyrill anamshukuru Mungu kwa upyaisho wa imani unaoendelea kujionesha kati ya waamini na kwamba, waamini wanaanza kugundua tena ndani mwao thamani ya imani na ibada!

Naye Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2016 anayaelekeza mawazo yake kwa Jumuiya za Kikristo zinazoendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia. Kuna mauaji ya kimbari yanayofanywa dhidi ya Wakristo huko Pakistan, jambo ambalo bado linafumbiwa macho na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa. Wahusika wa mauaji haya wanapaswa kufikishwa na kuwajibishwa mbele ya vyombo vya sheria. Askofu mkuu Welby anasema, licha ya madhulumu na nyanyaso dhidi ya Wakristo lakini mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimiwa katika: damu, huduma, sala na maisha ya kiroho unaendelea kushika kasi kubwa miongoni mwa Wakristo!Huu ni mwaliko wa kuendelea kuimarisha Uekumene wa huduma inayotekelezwa katika mwanga wa Fumbo la Umwilisho. Kuna haja ya kuendeleza mchakato wa umoja katika mateso na mahangaiko; umoja katika matumaini, ili kufikiri na kutenda kadiri ya mwanga na nguvu za Kristo Mkombozi wa dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.