2016-12-22 14:42:00

Zawadi kubwa ya Noeli ni Mtoto Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 22 Desemba 2016 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Vatican waliokuwa wameandamana na familia zao kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana heri na baraka kwa ajili ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2017. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema, baraka na karama mbali mbali ambazo amewakirimia waja wake na zawadi kubwa kuliko zote ya Kipindi cha Noeli ni Mtoto Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na kuzaliwa na Bikira Maria.

Baba Mtakatifu kwa niaba ya wafanyakazi wa Vatican anapenda pia kumshukuru Mungu kwa zawadi ya kazi ambayo ina mafao makubwa kwa wafanyakazi wenyewe pamoja na familia zao. Imekuwa ni fursa pia ya kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watu wasiokuwa na fursa za ajira sehemu mbali mbali za dunia; au watu wanaofanya kazi za suluba dhidi ya utu na heshima yao kama binadamu; watu wanaolipwa kiduchu pamoja na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa afya zao.

Kumbe, wale waliobahatika kupata fursa za ajira, waoneshe shukrani kwa Mungu kwa zawadi hii, kwa kuwajibika barabara, kwa kuboresha mazingira ya kazi; kwa kuwaheshimu na kuwathamini wafanyakazi wenyewe pamoja na familia zao katika misingi ya haki na utu! Wafanyakazi wa Vatican wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia Injili ya Kristo inayofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kila kitu kiweze kwenda kadiri ya sheria, kanuni na taratibu pasi na njia za mkato!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wafanyakazi wote wa Vatican na kuwataka waendelee kuboresha kazi zao kwa kufanya vyema zaidi! Amewatakia pole wagonjwa na kuwatia shime wenye wasi wasi kutokana na changamoto walizonazo kwenye familia zao. Kimsingi, wafanyakazi wengi wa Vatican wanafahamiana, ikilinganishwa na sehemu nyingine za kazi. Ni mahali ambapo utaratibu unapaswa kuzingatiwa, kwa kuboresha mapungufu yanayoweza kujitokeza na kufanya kazi kwa ushirikiano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamewawezesha kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, changamoto iliyoko mbele yao kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanatoa nafasi ya kumwilisha neema ya Mungu katika maisha yao ya kila siku katika mazingira ya familia, kazi na mahali popote pale walipo! Siku kuu ya Noeli ni chemchemi ya neema ya wokovu wa Mungu kwa watu wote, changamoto ni kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa: kiasi, haki na uchaji wa Mungu!

Hii inatokana na ukweli kwamba, Yesu Kristo ndiye neema inayofumbata upendo wa Mungu uliomwilishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini wamekirimiwa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu yanayopaswa kufanyiwa kazi kila siku kwa kuwa na kiasi, haki na uchaji wa Mungu! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi wa Vatican kumfikishia salam na matashi mema kwa watoto, wazee na wagonjwa wanaopaswa kusindikizwa daima kwa njia ya sala. Anawaombea ili Yesu aendelee kuwasha moto wa huruma ya Mungu katika maisha yao, Bikira Maria awalinde na kuwaombea kwa tunza yake ya Kimama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.