2016-12-17 15:11:00

Papa Francisko kutembelea Fatima tarehe 12-13 Mei 2017


Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki na Serikali ya Ureno kutembelea nchini humo, kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Karne Moja, tangu Bikira Maria wa Fatima alipowatokea watoto watatu wa Fatima, yaani Francis na Yacinta Marto na Lucia Dos Santos waliokuwa wakichunga kondeni, hawa wakawa ni vyombo na mashuhuda wa “Siri ya Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima”. Kumbe, Bikira Maria ni alama ya matumaini kwa sasa na kwa siku za baadaye!

Kwa ajili ya maadhimisho haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno limeandika Waraka wa Kichungaji kuhusiana na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto Watatu wa Fatima. Padre Emmanuel Joaquim Gomes Barbarosa, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno anasema, lengo la Waraka huu wa kichungaji ni kuisaidia familia ya Mungu nchini Ureno kumwilisha ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima sanjari na kukoleza mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani wenye mvuto na mashiko!

Maaskofu wanakazia pamoja na mambo mengine, ushuhuda wa kinabii, toba na wongofu wa ndani; mapambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo! Haya ni mambo makuu ambayo Bikira Maria aliwakabidhi Watoto Watatu wa Fatima. Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linasema, hili ni tukio kuu la imani kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Ni zawadi na mwaliko wa kumwilisha maadhimisho haya katika ngazi ya mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake. Kanisa nchini Ureno na ulimwengu katika ujumla wake linatumwa kutangaza na kushuhudia: amani, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake.

Kardinali Manuel Clemente, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno anakaza kusema, Waraka huu wa kichungaji ni tafakari na upembuzi wa kina mintarafu tukio kuu la imani lililotokea kunako mwaka 1917 na mwaliko kutoka kwa Bikira Maria ni kutubu na kuiamini Injili, yaani waamini waanze mchakato wa kurejea tena katika tunu msingi za Kiinjili. Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza, Bikira Maria aliwatokea Watoto watatu wa Fatima kunako tarehe 13 Mei 1917, kwenye Kijiji cha “Cova da Aria”, mjini Fatima.

Kunako mwaka 1930, Jimbo Katoliki la Leira, likaridhika kwamba, Watoto watatu wa Fatima, kweli walimwona Bikira Maria na huo ukawa ni mwanzo wa Ibada kwa Bikira Maria wa Fatima. Kunako mwaka 1942 Papa Pio wa XII akauweka ulimwengu wote chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Mtakatifu Yohane Paulo II anakiri kwamba,  ni kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima aliweza kunusurika kwa kifo baada ya kupigwa risasi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hapo tarehe 13 Mei 1981.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.