2016-12-17 07:16:00

Noeli ni Siku kuu ya Unyenyekevu!


Kardinali Angelo Comastri, mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 16 Desemba 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya sherehe ya Noeli kwa wafanyakazi wote wa Vatican. Anasema, Noeli ni Siku kuu kubwa kwa Wakristo, lakini ni Siku kuu inayofumbatwa katika unyenyekevu unaoshuhudiwa na Mtoto Yesu anayezaliwa kwenye Pango la kulishia wanyama. Katika mahubiri yake, amekazia kwamba, fadhila ya unyenyekevu ni tabia ya kawaida, imara na chachu ya kutenda mema na kutoa kilicho chema kutoka katika undani wa nafsi mtu.

Kardinali Comastri amewataka wafanyakazi wa Vatican kuwa na mwono na mwelekeo mpana zaidi katika maisha na utume wao kwani, ulimwengu ni mpana na wao ni sehemu ndogo tu ya ulimwengu wenye raha, taabu na changamoto zake. Kwa njia ya fadhila ya unyenyekevu, waamini wanaweza kutambua na kuthamini ukuu wa Mungu katika maisha yao, kwani Yeye ni mwanzo na mwisho, Alfa na Omega, nyakati zote ni zake. Sayansi ya anga ni fundisho kubwa kwa mwanadamu kutambua kwamba, kuna mambo makubwa zaidi, hata pengine kuliko sayari ya dunia hii.

Yesu Kristo, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, alizaliwa katika hali ya umaskini na unyenyekevu; akalazwa katika Pango la kulishia wanyama, kwani wazazi wake walikosa nafasi kwenye nyumba za wageni pale mjini Bethlehemu. Katika ukuu na utukufu wake, akajinyenyekesha na kuzaliwa kwake Bikira Maria na wala hakuona kuwa sawa na Mungu ni jambo la kung’ang’ania sana. Kwa bahati mbaya anasema Kardinali Comastri, leo hii duniani kuna watu wanataka kujikuza na kujifanya kuwa ni “miungu watu”. Hawa wamejaa kiburi, maringo na majivuno.

Dunia inaweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, ikiwa kama fadhila ya unyenyekevu itaweza kumwilishwa katika vipaumbele na maisha ya watu wengi duniani. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni matokeo ya kukosekana kwa fadhila ya unyenyekevu na badala yake, wakuu wa mataifa “wanatunishiana misuri” lakini wanaoteseka ni maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Ibada hii imehudhuriwa na waamini walei, watawa na wakleri wanaofanya kazi na utume wao mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.