2016-12-15 14:36:00

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza Mameya!


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi kuanzia tarehe 9-10 Desemba 2016 iliendesha mkutano wa kimataifa uliowashirikisha wastahiki Mameya kutoka katika miji mikuu Barani Ulaya. Mkutano huu uliongozwa na kauli mbiu “Bara la Ulaya: wakimbizi ni ndugu zetu”. Mkutano huu ulijadili tema mbali mbali ambazo zimekuwa zikipewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baada ya mkutano huo, Baba Mtakatifu amewandikia barua ya shukrani wastahiki mameya na kuwatia moyo kuendelea kujikita katika ujenzi wa mtandao wa mshikamano na huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, amefuatilia kwa ukaribu sana majadiliano yaliyofanywa na Mameya hawa pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana baada ya mkutano huu, kwa kuunda mtandao wa mshikamano wa huduma ya upendo miongoni mwa Mameya ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya.

Baba Mtakatifu anamshukuru kila meya mmoja mmoja kwa kutumia akili, hekima, busara na ujasiri kwa ajili ya kuunda mtandao utakaosaidia kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Anapenda kuwahakikishia Mameya hawa kuwa mlango wake daima utaendelea kuwa wazi ili kuendeleza ushirikisho na mshikamano wa huduma kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaomba Mameya kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka yao.

Msemaji mkuu wa Vatican Dr. Greg Burke anafafanua kwamba, barua hii ya Baba Mtakatifu kwa Mameya wa miji mikuu ya Bara la Ulaya imetfasiriwa kwa lugha mbali mbali na kutiwa sahihi na Baba Mtakatifu kwa mkono wake mwenyewe, ili kuonesha uzito wa mshikamano huu wa huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.