2016-12-10 07:22:00

Masista wa Ivrea iweni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini


Watawa wa Shirika la Upendo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea maarufu kwa jina la “Masista wa Ivrea” wamehaswa juu ya utume wao wa kuwa mashahidi wa upendo wa Mungu kwa maskini zaidi katika ulimwengu mamboleo. Wito huo umetolewa na Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Ndoa na familia ya Yohane Paulo II wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2016. Ibada hii imefanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria, Trastevere, Jimbo kuu la Roma, Italia na imekwenda sanjari na watawa nane wa Shirika hili kuweka nadhiri zao za daima.

Askofu Mkuu Paglia amesema: “Mmechaguliwa ili muwe mashahidi wa upendo kwa maskini zaidi ndiyo maana hakuna wakati mwingine kama leo hii mnapoweza kuukwepa utume huo. Tupo katika ulimwengu ambao umejikinai wenyewe na kuusukumia kando upendo halisi wa Mungu, ulimwengu unaoonekana kuegemea zaidi katika kujilimbikizia: utajiri na mali; ulimwengu unaogelea katika hali ya kujisikiliza wenyewe. Hapo ndipo mnapoitikia “Ndiyo yenu, ili kwenda kutumikia na kuifanya sauti ya upendo wa Mungu ipenye kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Mnatumwa kwenda kwa watu walio pembezoni  ili kuwaonesha uzuri wa Mungu”.

Maisha ya utawa yanamdai mmoja kujiweka wakfu na kumdhihirisha Kristo na upendo wake kwa watu wengine. Askofu Mkuu Paglia aliyaunganisha majitoleo yao hayo na Fumbo la Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili akisema kwamba “Maria ni Imakulata ndiyo maana anambeba Yesu katika mikono yake” Akaendelea kukazia kwamba “hiyo ndiyo maana ya Fumbo la kukingiwa dhambi ya asili, yule ambaye anawajibika kumbeba Yesu anapaswa kutakaswa na dhambi”. Na kisha akawaelezea haiba inayopaswa kuwepo ndani mwao kwa kuupokea ujumbe wa Mungu, haiba ya unyenyekevu huku akimwelezea Bikira Maria kama mmoja aliyefanikiwa kuubeba ujumbe wa Mungu “si kwa sababu  mastahili yake bali alikuwa ni mtumishi mnyenyekevu” na hivyo akawatia nguvu Watawa hao kwa kuwaambia kwamba  “ni Mungu pekee anayewawezesha bila ya mastahili yenu kusudi muweze kuueneza upendo wa Kristo kwa maskini”.

Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelii Gaudium” “Furaha ya Injili” alibainisha wajibu wa Kanisa na wanakanisa wa kuwahudumia maskini mithili ya upendo wa Baba mwenye huruma katika mfano wa mwanampotevu ambaye alikuwa ameuacha wazi mlango wa moyo wake tayari kumpokea kwa upendo mwanaye anayerudi kwake huku akiwa na shahuku ya kuuonja upendo wake. Katika roho hiyo ya moyo ulio na utayari Baba Mtakatifu anasema: “Haya twendeni sasa, twendeni tukamgawie kila mmoja uzima utokao kwa Yesu Kristo ... ninahitaji zaidi Kanisa ambalo limechubuliwa, limejeruhiwa na limechafuka kwa sababu tu limekuwa tayari kutoka nje kuliko kuwa na Kanisa lisilo na siha kutokana na kujifungia na kung’ang’ania usalama wake” (EG 49).

Askofu Mkuu Paglia aliunganisha Fumbo la Bikira Maria kukingiwa dhambi ya Asili na matendo makuu ya Mungu. Akisema: “Sherehe ya Bikira Maria Imakulata kabla ya kuwa sherehe ya Mama yetu ilikuwa ni tendo la Mungu mwenyewe aliyenyanyua macho yake kwa mtumishi wake na tangu mwanzo mara baada tu ya kutungwa mimba, wakati akiwa hajui lolote, kwa uchaguzi wake na upendo wake anamkinga na dhambi ya asili”. Hivyo, akawakumbusha kuwa kuitikia kwao sauti hiyo ya Mungu na kutaka kujikabidhisha kwake kwa maisha yao yote kutapata nguvu kama kutaeleweka katika muono huu wa kimungu kwani “kuna muunganiko kati ya ndiyo ya Maria kwa Mungu na ndiyo ya hawa dada zetu ambayo wanadhamiria kuifanya mbele ya Mungu”.

Ndiyo yao ya leo inaunganishwa na utayari  wa kuifanya sauti ya Mungu kuwa na nafasi katika nafsi zao mithili ya Bikira Maria na hivyo kutoa jibu kwa hofu na ukosefu ambao humtawala mwanadamu pale anapoiacha sauti ya Mungu kama Adam na Eva kwani “kuna tofauti kati ya Adam na Eva ambao wanajificha, wana hofu, wanajisikia wapo utupu , utupu wa upendo, utupu wa kupata kuangaliwa na wengine” kwa sababu tu waliacha kuiskiliza na kuitii sauti ya Mungu.

Watawa waliweka nadhiri zao za daima mbele ya Mama Mkuu wa Shirika hilo Sr. Palma Porro na kushuhudiwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki. Watawa walioweka nadhiri zao za daima kutoka Tanzania na Kenya ni: Sr. Marcelina Mahiri Pius, Sr. Genoveva Thomas Mathonya Mapalasha, Sr. Odilia Fridolin Joseph Mgogo, Sr. Flora John Ndyani, Sr. Julia Achieng’ Okong’o, Sr. Margaret Odhiambo Onywera, Sr. Prisca Honoratus Mhamilawa na Sr. Cresensia Peter Mushi. Shirika la Mapendo la Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili lilianzishwa mwanzoni mwa karne ya 19 katika mkoa wa Piemonte Kaskazini mwa nchi ya Italia na Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna likijikita zaidi katika huduma kwa maskini kwa moyo wa kujitolea bila kujibakiza.

Watawa hawa wanaendelea kutoa huduma zao sehemu mbalimbali duniani hasa katika shule, hospitali na vituo mbalimbali vya matendo ya huruma kwa wahitaji. Barani Afrika wanafanya utume wao nchini Tanzania, Kenya na kwa bahati mbaya kutokana na vita na hali kuendelea tete kwa ajili ya usalama na maisha ya watawa, Shirika liliamua kusitisha huduma yake kwenye hospitali za Libya ambako wamekuwa huko kama mashuhuda wa upendo kwa miaka zaidi ya hamsini!

Na Padre Joseph Peter Mosha.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.