2016-12-09 08:14:00

Sikilizeni kilio na mahangaiko ya wagonjwa na maskini Kenya!


Wafanyakazi katika sekta ya afya nchini Kenya, Alhamisi tarehe 8 Desemba 2016 waliamua kufanya mgomo na maandamano makubwa Jijini Nairobi, ili kuishinikiza Serikali ya Kenya kuwaongezea mshahara na kuwaboreshea mazingira ya kazi sanjari na kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma unaopelekea Serikali kuyalipa makampuni makubwa fedha nyingi zinazonuka rushwa na ufisadi. Waziri wa afya kwa sasa anachunguzwa na vyombo vya sheria kutokana na tuhuma za rushwa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa kuguswa na mahangaiko ya wagonjwa wanawaomba wafanyakazi katika sekta ya afya kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wagonjwa na maskini wanaohitaji huduma yao, ili kuokoa kwanza kabisa maisha ya watu kuliko kitu kingine chochote kile. Kuna wazee, akina mama wajawazito, kuna watoto na wagonjwa walioko kufani wanahitaji huduma makini, lakini kwa bahati mbaya wote hawa wametelekezwa hospitalini pasi na msaada.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kimsingi linakubaliana na hoja zilizotolewa na wafanyakazi katika sekta ya afya na kwamba, linasikitika kuona kwamba, Serikali imeshindwa kutekeleza makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa. Lakini, Maaskofu wanasema si haki kuwatelekeza wagonjwa katika mahangaiko haya makubwa kama shinikizo la madai yao. Wafanyakazi katika sekta ya afya wanadhamana ya kulinda na kudumisha maisha ya binadamu, lakini vitendo vya sasa vinahatarisha maisha ya watu. Inasikitisha kuona kwamba, Serikali inaendelea kufumbia macho migomo hii badala ya kuitafutia suluhu ya kudumu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawaomba wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa afya za wananchi pamoja na kuendelea kutengeneza mazingira ya majadiliano ili kupata ufumbuzi wa changamoto hii inayotishia maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Migomo haiwezi kukubali kuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida wakati kuna watu wanaoendelea kupoteza maisha yao pasi na huduma. Maisha ya binadamu ni matakatifu na yana thamani kubwa kuliko mradi wowote ule.

Maaskofu Katoliki Kenya wanawataka wataalam na wafanyakazi katika sekta ya afya kuingilia kati ili kuokoa maisha ya watu kama sehemu ya utekelezaji wa kiapo chao cha kazi na maadili yanayopania kulinda maisha ya watu. Huduma za matibabu zirejeshwe haraka iwezekano pasi na kuchelewa sana. Changamoto hii iwe ni nafasi kwa hospitali binafsi kusaidia kutoa huduma wakati huu wa kipindi cha dharura ili kuokoa maisha. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwamba, hatua madhubuti zitaweza kuchukuliwa ili kurejesha tena huduma ya afya katika hali yake ya kawaida!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.