2016-12-08 08:23:00

Siku kuu ya B.M. Mkingiwa Dhambi ya Asili Msimamizi wa Tanzania


Ilikuwa ni tarehe 8 Novemba 1984, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka unaojulikana kama “Tot Tantaeque” yaani “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Hili ni ombi lililotolewa kwa wakati huo na Askofu Anthony Mayala aliyekuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kuomba ili Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili aweze kuwa msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia familia ya Mungu nafasi ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhuru, siku moja tu, baada ya kuadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mkutano wake mkuu wa mwaka uliofanyika Juni 2016 liliamua kwamba, kuanzia sasa Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili itakuwa inaadhimishwa kitaifa nchini ifikapo tarehe 9 Desemba. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika barua yake kwa ajili ya tukio hili anasema, uamuzi huu ni utekelezaji wa zawadi iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1984 kwa kuiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Kumbe, kwa mara ya kwanza, katika historia ya Tanzania, Siku kuu ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili kitaifa nchini Tanzania inaadhimishwa rasmi tarehe 9 Desemba 2016. Hii ni nafasi ya kuombea familia ya Mungu nchini Tanzania ili iweze kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, nguzo msingi ambazo daima zimewatambulisha watanzania katika Jumuiya ya Kimataifa.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania kunako mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezesha watanzania kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria ziwe ni kwa ajili ya mafao ya wengi. Aliwaombea Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu. Aliwaombea upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila, utaifa ili watanzania wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanzania na majirani zake; viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.