2016-12-05 09:11:00

Ushuhuda wa Injili ya Familia Barani Asia


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, Fabc, limehitimisha mkutano wake mkuu wa kumi na moja uliofunguliwa hapo tarehe 28 Novemba hadi tarehe 4 Desemba 2016 kwa kuwashirikisha wawakilishi kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia. Mkutano huu umeadhimishwa huko Colombo, Sri Lanka na Kardinali Telesphore Placidus Toppo, amemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; vita, dhuluma na nyanyaso za Wakristo huko Mashariki ya Kati hususan nchini Siria ni kati ya mada zilizopewa kipaumbele cha kwanza na wajumbe wa mkutano huu.

Wajumbe wa mkutano huu wanasema, inasikitisha kuona kwamba, Wakristo wanateseka na kunyanyasika hata katika nchi zao wenyewe. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zimejadiliwa mintarafu mwanga wa huruma na upendo wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu. Hii ni tema ambayo bado inatoa mwangwi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliofungwa hivi karibuni.

Wajumbe wamepembua kwa kina mapana sera na mikakati itakayoziwezesha familia Barani Asia kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za Injili ya familia. Itakumbukwa kwamba, mkutano huu, umeongozwa na kauli mbiu “Familia ya Kikatoliki Barani Asia: Kanisa mahalia maskini katika utume wa huruma ya Mungu”. Ibada ya Misa ya ufunguzi, iliongozwa na Kardinali Telesphore Placidus Toppo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ranchi, India aliyewataka viongozi wa Kanisa na wadau wa shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa familia Barani Ulaya, kutobweteka na hali yao, bali wajitose kimasomaso kwenda nje ili kushiriki katika mchakato wa maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya familia, kiini cha Uinjilishaji na chachu ya mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Anasema, Kanisa Barani Asia ni Kanisa dogo la nyumbani ambalo ni maskini lakini linaweza kuwa ni chombo na shuhuda wa utume wa huruma ya Mungu kwa waja wake, katika Bara la Asia ambalo lina matatizo, changamoto na fursa mbali mbali za kufanyiwa kazi kwa ajili ya kuendeleza utume wa maisha ya ndoa na familia.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Pierre Nguyen Van Tot, Balozi wa Vatican nchini Sri Lanka pamoja na wawezeshaji wakuu kwenye mkutano huu wamelitaka Kanisa Barani Asia kufungua malango ya Kanisa, Sakramenti na upendo kwa watu wanaotaka kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kanisa lisimame kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza maskini na wanyonge ndani ya jamii. Wajumbe wamebainisha mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji utakaoliwezesha Kanisa Barani Asia kuwa kweli mhudumu wa Injili ya Familia Barani Asia, ambako idadi ya Wakatoliki ni sawa na asilimia 3% ya idadi ya watu wote wanaoishi Barani Asia.

Changamoto kubwa kwa familia Barani Ulaya ni: Ukosefu wa uaminifu, ugumba, uchumba sugu, ongezeko kubwa la talaka, utengano wa muda mrefu wa wanandoa kutokana na kazi, nyanyaso za kijinsia, utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini pamoja na wimbi kubwa la wahamiaji wanaokimbia kutoka Asia ili kutafuta maisha bora sehemu mbali mbali za dunia.

Itakumbukwa kwamba, tema ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia imekuwa ikipewa kipaumbele cha pekee na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia katika maisha na utume wake tangu mwaka 1972 lilipoanzishwa. Kwa mwaka huu 2016, familia Barani Asia zimekuwa zikihamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa Injili ya uhai pamoja na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.