Huruma na amani, huu ni mwaliko wa baba Mtakatifu Francisko, kwa watu wote wenye mapenzi mema, ili kupata kutualika kuishi huruma na amani, na mwaliko huu unakuja tu mara baada ya hitimisho la mwaka wa huruma ya Mungu. Mwaliko huu wa baba mtakatifu umeletwa kwetu na barua yake ya kitume ijulikanayo “Misericordia et misera” yaani "Huruma na amani". Neno huruma na amani kama ilivyotumiwa na Baba Mtakatifu, ni neno lilokwisha tumiwa tena na Mtakatifu Agustino alipokuwa akioanisha maneno ya Yesu alipokutana na Yule mwanamke mzinzi ( Yn 8:11). Na hapa Baba mtakatifu anatuambia tendo la Yesu kumsamehe yule mwanamke mzinzi ni jambo la upendo wa Mungu, katika kuwafikia hata wadhambi na wenye kutubu, na hii ni huruma katika uhalisia wake, anasema baba Mtakatifu.
Baba Mtakatifu katika waraka huu wa kitume anaendelea kunukuu kifungu cha Injili chenye kumsamehe yule mwanamke mzinzi, kwani kifungu hiki kinasimama kama alama ya huruma ya Mungu katika msamaha. Jambo ambalo lilionekana sana katika maadhimisho ya mwaka mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambapo maadhimisho yake yataendelea kutuweka wapya na wenye upendo katika jamii zetu na hivyo kutuwezesha kutembea katika upendo na msamaha , kama yule mwanamke alivyoambiwa na Yesu, nenda na kuanzia sasa usitende dhambi tena.
Baba Mtakatifu katika waraka wake huu wa kitume, Huruma na amani anaelezea pia na kusisistizia umuhimu wa msamaha, na anasema kila Injili imejaa msamaha kama alama ya upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Ni katika utajiri huu wa huruma ya Kimungu, Yesu anaalikwa kwenye chakula katika nyumba ya mfarisayo na hapo anajitokeza mwanamke ambaye kila mmoja alimfahamu kuwa ni mzinzi, ambapo mwanamke huyu anamkaribia Yesu na anaosha miguu ya Yesu kwa machozi yake na kukausha miguu ya Yesu kwa nywele zake, na ndipo Yesu kwa kuwaangalia wale Mafarisayo, akamwambie Yule mwanamke, dhambi zako zimesamehewa.
Msamaha huu haukuishia hapa tu, bali Baba Mtakatifu anaendelea kusema , msamaha wa Yesu uliendelea hadi nyakati za mwisho pale Msalabani, Yesu alipotamka maneno haya ya msamaha, baba uwasamehe kwani hawajui watendalo. Na msamaha huu unaendelea hadi sasa. Sasa ni sisi kuupokea, kuuishi na kumshukuru Mungu daima. Baba Mtakatifu anatuambia huruma ya Mungu haina mwisho, wala haina mipaka, anasema huruma hii ipo kizazi hata kizazi na inaendelea kuwepo daima hasa kwa wale wanaomtumainia Mungu kama muumba wao bila kuchoka.
Baba Mtakatifu pia anatuelekeza kujifunza furaha itokanayo na msamaha , kwani furaha hii ni chanzo cha upendo wa Mungu na upendo huu unatusaidia kuondokana na ubaguzi, pamoja na uchoyo na hivyo kutufanya kuwa vyombo vya huruma ya Mungu. Anatuasa kuwa ili kupata furaha nafsini mwetu yatupasa kuondokana na utamaduni uliokandamizwa na teknolojia , uchungu na upweke, na badala yake yafaa kujipa matumaini na furaha ya kweli, na hii ni furaha itokanayo na moyo wenye huruma na hapa ndipo tutakapopata kuungana na maneno ya matakatifu Paulo yasemayo; siku zote, tena nasema siku zote furahini katika Bwana. Ndugu yangu msikilizaji, Mwaka Mtakatifu wa Jubilee ya huruma ya Mungu , umeeisha na huu ukiwa ni mwaliko wa kutufanya tuangalie mbele katika furaha, katika uaminifu na katika mwonekano mpya na huku tukijichotea utajiri wa huruma na amani.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Pd. Agapiti Amani, ALCP.OSS.
All the contents on this site are copyrighted ©. |