2016-12-05 14:11:00

Caritas Hispania na utandawazi wa mshikamano


Tumeitwa kuwa Jumuiya, hii ni kauli mbiu ya Caritas Hispania kwa mwaka wa Kanisa 2016-2017. Lengo ni kushirikisha jumuiya mahalia katika kubadilika na kutafuta haki jamii. Shirikisho hilo la Iberia Hispania, kwa miaka mitatu sasa limenuia kuwaamsha watu nchini Hispania kupenda na kuishi haki. Kwa mwaka 2014-2015, kauli mbiu ilikuwa, unafanya nini na ndugu yako?, kwa mwaka 2015-2016 kauli mbiu ilkuwa, tenda haki acha ndoto zako. Caritas Hispania ipo kwenye harakati za kujenga jumuiya na mshikamano kati ya watu katika makazi na sehemu za kazi. Ni tumaini lake kuwa utendaji huo utawafanya watu kuingia katika ulimwengu wa upendo, mshikamano, haki, udugu kiasi cha kubadili na kutajirisha matumaini ya watu.

Wahamiaji, mabadiliko ya tabia nchi, haki za binadamu, na mshikamano kati ya watu, ni nyanja za msingi zinazozingatiwa wakati Caritas Hispania wanaaadhimisha kwa namna ya pekee katika sikukuu za Noeli na Ekaristi Takatifu. Utendaji huo unawasaidia watu wa mataifa, kabila na tamaduni mbali mbali kuishi pamoja kwa upendo. Katika kuishi pamoja kwa mshikamano wananuia kulinda mazingira, kwani hakuna yeyote mwenye haki ya kuharibu mazingira kwa faida zake binafsi, kwa haya yote haki za kila mwanadamu lazima zilindwe, awe ni rai au mgeni. Udugu na mshikamano ni kiini katika yote, kwani ni kwa namna hii jamii itaweza kubadilika na kila mmoja kushiriki na kupokelewa kwa heshima. Caritas wanalo tumaini kubwa la kuifanya Hispania kuwa ni jumuiya ambamo kila mmoja anawajibika kwa ajili ya kila mmoja, na tabia za ubinafsi zinatokomezwa.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.