2016-12-03 08:58:00

Wanafunzi pambaneni kikamilifu na changamoto za kimaadili!


Kongamano la IV la Shughuli za kichungaji Kimataifa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, kuanzia tarehe 28 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2016, ilikuwa ni nafasi ya kuwafunda vijana ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda na wajenzi wa jamii bora zaidi ya binadamu! Itakumbukwa kwamba, Kongamano hili lilikuwa linaongozwa na kauli mbiu “Waraka wa Furaha ya Injili na changamoto za kimaadili katika ulimwengu wa wasomi wa vyuo vikuu kimataifa mwelekeo wa jamii bora zaidi”.

Wanafunzi 130 kutoka katika nchi 36 duniani wameshiriki, kati yao kulikuwepo na wanafunzi 30 wanaoishi na kusoma nje kabisa ya nchi zao wenyewe. Taarifa zinaonesha kwamba, leo hii kuna zaidi ya wanafunzi millioni tano wanaoacha nchi zao asilia na kwenda kujiendeleza katika elimu ya juu kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kimataifa. Lengo msingi la kongamano hili, lilikuwa ni kupembua kwa kina na mapana uhimizaji, tafakari na mchanganuo wa Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Injili kama msingi wa shughuli za kichungaji maridhiwa na zinazokwenda na wakati!

Wadau wa shughuli za kichungaji kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameshiriki katika kongamano hili pamoja na kuchambua kwa kina na mapana: changamoto za kitamaduni, kidini, kiimani, kiutu zinazojitokeza katika mazingira ya vyuo vikuu mintarafu sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kimataifa. Wahusika wakuu katika kongamano hili walikuwa ni wanafunzi wenyewe, walioshirikisha ushuhuda, tafakari pamoja na kuchangia kwa kina na mapana mijadala iliyoendeshwa kwenye makundi ya wanafunzi.

Wanafunzi wamegusia umuhimu wa kuwa na sera na mikakati ya kichungaji itakayosaidia kuwaongoza na kuwaelekeza wanafunzi wa vyuo vikuu kimataifa, lengo na majukumu yaliyobainishwa kwenye kongamano hili. Kwa njia hii, itakuwa ni rahisi kwa wanafunzi wenyewe kumwilisha changamoto hizi pamoja na kuibua mwelekeo mpya, ili kuwasaidia vijana kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya mchakato wa mageuzi katika jamii na mshikamano wa upendo na wanafunzi kutoka katika dini na imani tofauti.

Walezi na wanafunzi wenyewe wamesema, kuna haja ya kuendelea kuwahamasisha wanafunzi kutoka taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kimataifa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Furaha ya Injili kama chachu makini ya Uinjilishaji. Wanafunzi hawa wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa katika nchi zinazowahifadhi, ili kushirikishana fursa, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao kama wanafunzi.

Wanafunzi wajibidishe zaidi ili wasitumbukie katika ombwe la upweke hasi unaoweza kuwasababishia msongo wa mawazo na hata kukata tamaa. Wanafunzi wameshuhudia haya wakati wa kongamano hili ambalo pia lilipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wanafunzi wanawataka viongozi wa maisha ya kiroho kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kuwa ni rejea kwa wanafunzi wanaotoka nje ya nchi zao ili kuweza kujumuishwa katika mtandao wa mahusiano mapya yanayojikita katika imani.

Baadhi ya wanafunzi wameshuhudia jinsi ambavyo wamepokelewa kwa mikono miwili katika Jumuiya za waamini na kushirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Kumbe, Jumuiya za waamini zioneshe ari na moyo wa ukarimu kwa wanafunzi wageni, ili kusaidia mchakato wa malezi na makuzi endelevu katika maisha ya kiroho kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kimataifa. Wajumbe kutoka Makanisa mbali mbali ya Kikristo wameshiriki pia katika kongamano hili kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene bila kusahau ujumbe wa wanafunzi kutoka katika dini mbali mbali duniani. Lengo ni kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini hata miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, kujenga na kudumisha Jamii bora zaidi inayojikita katika msingi wa haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Kilele cha maadhimisho ya Kongamano hili ni pale, wajumbe walipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baadhi yao wakabahatika kupiga naye picha za kumbu kumbu ya kongamano hili; tayari kutoka kifua mbele ili kwenda kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili kwa Watu wa Mataifa. Wametakiwa kuwa “ngangari” na kamwe wasiogope changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao. Majaalim na walezi, wasaidie kuwafunda vijana kuthamini na kumwilisha kanuni maadili katika maisha yao. Vijana wasomi wasaidiwe na Jamii kupata fursa za ajira ili waweze kuchangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya nchi zao. Baba Mtakatifu anasema, inasikitisha kuona vijana baada ya kusomeshwa na Jamii kwa gharama na sadaka kubwa, wanazikimbia nchi zao ili kutafuta fursa bora zaidi za ”kijani kibichi” kwa vile tu, hawakupata nafasi ya kushirikishwa kikamilifu na Jamii zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.