2016-12-03 07:31:00

Papa akutana na kuzungumza na Rais wa Uruguay!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 2 Desemba 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Tabarè Ramòn Vazques Rosas wa Jamhuri ya Watu wa Uruguay, ambaye baadaye alipata nafasi ya kukutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao, wameridhishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Paraguay pamoja na pande hizi mbili kuendelea kujizatiti kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na amani jamii. Katika mazingira kama haya, viongozi hawa wamebainisha mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wengi nchini Uruguay hususan katika maendeleo endelevu, elimu na huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo na mgeni wake, wamegusia pia masuala ya kisiasa katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa, mintarafu ukuaji wa taasisi za kidemokrasia, hali ya kijamii na kibinadamu huko Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.