2016-12-03 12:14:00

Komesheni tabia ya kuwageuza watoto kuwa chambo cha vita!


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye katika nia yake ya jumla kwa ajili ya Mwezi Desemba, 2016 inayokemea utumwa wa watoto wadogo wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo wakati wa vita. Nia hii ya Baba Mtakatifu kwa njia ya video imesambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala kwa kumwonesha mtoto ambaye amevikwa magwanda ya kijeshi na kupambwa kwa risasi, tayari kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita!

Mtoto huyu anajitambulisha na kujionesha hadharani! Huyu ni mtoto ambaye maisha yake yako hatarini, badala ya kuwa mstari wa mbele kama chambo cha vita, alipaswa kuwa darasani akisoma; kuwa uwanjani akicheza na watoto wenzake; kuwa kwenye familia akipata malezi na tunza ya familia yake, lakini kwa bahati mbaya, dunia imemgeuzia kisogo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ulimwengu huu ambao umeendelea kwa sayansi na teknolojia, umejikita katika biashara haramu ya silaha zinaoishia mikononi mwa watoto ambao wanapandikiza utamaduni wa kifo! Hawa ni watoto ambao kifo kiko usoni mwao wakati wowote wa maisha yao! Umefika wakati kwa watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kuokoa na kulinda maisha, utu na heshima ya watoto hawa pamoja na kuhakikisha kwamba, utumwa dhidi ya watoto hawa unakomeshwa, ili kuwapatia fursa ya  kuanza kuandika upya kurasa safi za historia na maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.