2016-12-03 14:45:00

Dumisheni amani ya kweli kwa toba na wongofu wa ndani!


Katika dominika hii ya pili ya majilio dhamira inayotuongoza inahusu amani ya kweli. Ile amani itokayo mbinguni. Tunaona katika injili Yesu akiongea na mtangulizi wake – Yohane Mbatizaji.  Katika Isaya 40:3 – tunasoma hivi: Mtu analia. Tengenezeni jangwani njia ya Bwana. Nyoosheni nyikani barabara kwa Mungu wetu. Kiini cha mafundisho ya Yohani kipo katika neno hili la Nabii Isaya.

Yohane alihubiri katika jangwa la Yudea. Tunaweza kufananisha jangwa hilo na mazingira yetu yanayotuzunguka na hali zetu na yote yaliyopo. Pengine leo tunatakiwa tuingie na kuangalia mazingira yanayotuzunguka. Mwanadamu kafungwa na hali mbalimbali za ulimwengu. Yohane na Isaya wanazungumzia hali mbalimbali ambazo humzuia mwanadamu kumpata Mungu. Yohane anaongea juu ya mabonde na milima. Kwa wakati wetu huu tunaweza kuzifananisha na hali kama kiburi, uvivu, uchoyo, ukatili, tamaa ya fedha, uongo, kukengeuka, kukosa adabu, kutokujali, ulevi wa kila aina kama majivuno, ubinafsi n.k. Haya ni mambo ambayo humzuia mwanadamu kumpata Mungu katika maisha yake! 

Huku kuinyoosha njia kwatuita kujipanga upya. Yahitajika wongofu wa ndani. Hatuna budi kuhuisha dhamiri zetu. Tunaalikwa kufanya tafakari ya maisha yetu. Katika adhimisho la Ekaristi Takatifu, tunafanya tendo la kukumbuka. Bila kumbukumbu tungepoteza umimi wetu, kitambulisho binafsi. Mwenye ugonjwa wa amnesia hupoteza kabisa mwelekeo, hajui alipo, hana kumbukumbu na hata hakumbuki jina lake au mahali alipo. Kumbukumbu ikiungana na akili inaelekea kitu fulani halisi.

Utajiri wa mtu, familia, kabila, taifa haupimwi na wingi wa dhahabu au utajiri wa mali alizonazo bali wingi wa kumbukumbu walizo nazo katika dhamiri na matendo yao. Hatari ya kumbukumbu ni pale inapokuwa ng’ang’anizi. Kulazimisha mambo au kufanya kwa mazoea. Hatuna budi leo tunaposikia tena neno la Mungu na mwaliko wake kujipanga upya. Kuachana na mambo ng’ang’nizi ambayo hayana tija kwa ajili ya wokovu wetu na ulimwengu mzima.

Amani ya kweli hujengeka ikianzia ndani ya mioyo yetu. Nabii Isaya alikuwa mtu wa maono ya mbali. Yeye hafungwi na hali inayomfanya mwanadamu ajisikie mkiwa au kufungwa na hali yake n.k. anaona uwezekano wa kuanza upya - Isa. 11:6 ….mbwa mwitu atakaa pamoja na mwanakondoo, chui atalala karibu na mwanambuzi, ndama na mwanasimba watakuwa pamoja. Huu ndio wito wa neno la Mungu siku hii ya leo. Uwezekano wa yote kuwa mapya. Hii hali mpya itatutupatia nafasi ya kukaa pamoja na bila ubaguzi wo wote. Kil mmoja au kila kiumbe kitapata nafasi katika maisha yetu. Hii itawezekana tu kama tutakuwa tayari kuvaa sura ya Mungu na kuondoa sura zinazopingana na mapenzi yake Mungu. Tukifikia hali hiyo tutaweza kukaa pamoja bila utengano.

Kwa hakika wengi wetu inatuwia vigumu kutambua au kukiri dhambi au kuwajibika kwa makosa/dhambi zetu mbalimbali tunazotenda. Wengi wetu tumefungwa na hali yetu ya zamani na hivyo uwezekano wa kuanza upya ukawa mgumu. Mojawapo ya mifano iliyo wazi katika Biblia ni ile dhambi aliyotenda mfalme Daudi. Hata wakati nabii Nathan anamsimulia ule mfano, yeye hakung’amua kuwa ulimhusu yeye na dhambi aliyotenda. Na jibu lake Daudi ni kuwa mtu huyo anastahili kufa. Na haya ndiyo majibu tutoayo hata sisi tunapowahukumu wengine. Ni baada tu ya nabii kumwambia kuwa mtu huyo ni wewe, basi anarudi katika fahamu zake. Bahati yake Daudi alikiri kosa lake na kuomba msamaha. Wengi wetu tunashindwa kabisa kujitambua hata baada ya kuelezwa makosa yetu.

Ndugu zangu, kipindi cha majilio ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini. Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu - tunatafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu akaupa umaana uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu, akatuonesha maana ya maisha ya Kimungu - eti Mungu akawa mwanadamu. Tumshukuru Mungu. Tunatumainia ujio mtakatifu aliotuahidia, jumuiya takatifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu.  Kumbukumbu zinaamsha matumaini. Tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu, akakaa nasi na tunahuisha matumaini yetu kwamba Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Tunapata nafasi ya kumbuka matendo makuu ya Mungu na tunatumainia upendo mkuu wa Mungu. Ni kipindi cha kumbukumbu kinachotuwajibisha sana. Hata kama tumepoteza matumaini lakini kumbukumbu ya kimungu bado ipo. Ni muda wa kujirudi kama tutakuwa tumepotoka. Kukumbuka na kutumaini. Tukiwekeza katika Kristo, tutaweza yote.

Wakati wa utawala wa Napoleone mfungwa Mpolishi alikuwa amewekewa alama ya utambulisho ”N” katika kiganja chake. Alama hii ilimtambulisha kama mtumwa na bwana wake alimtumia apendavyo. Alipoelewa tu kuwa alama ile ilimtambulisha kama mfungwa/mtumwa, aliaamua kukata kiganja chake ili abaki huru. Na tangu siku hiyo akawa huru. Nasi pia tujichunguze kuona ni kitu gani kinachotufanya kuwa wafungwa na kuwa tayari kukiondoa hata kama kwa gharama kubwa.

Ndugu zangu, Mungu hatudai yanayopita uwezo wetu. Anatujua tulivyo na ndiyo maana anataka sisi tutoke katika hali zetu na kuingia katika uhalisia wa maisha.  Tunasoma katika Baruk 5:9 – neno hili la faraja “Maana Mungu ataongoza Israeli kwa furaha katika mwanga wa utukufu wake, kwa huruma na haki vitokavyo kwake”. Na Mtakatifu Agustino anasema kuwa Mungu ametuumba bila hiari au msaada wetu lakini kuupata wokovu yahitaji msaada wetu, juhudi binafsi. Tukiwekeza na Mungu hakika tutashinda yote na yote yatakuwa mapya na kuundwa upya.

Tumsifu Yesu Kristo.   

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.