2016-12-02 09:05:00

Uekumene wa sala kwa ajili ya huduma ya upendo na mshikamano!


Takribani miaka 50 iliyopita, Mwenyeheri Paulo VI na Patriaki Athenagora wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli walianzisha mchakato wa kutembeleana kama njia ya kuimarisha majadiliano ya kiekumene, changamoto iliyokuwa imeanzishwa punde tu na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Huo ukawa ni mwanzo wa safari ya majadiliano ya kitaalimungu kati ya Makanisa haya mawili sanjari na uundwaji wa tume ya pamoja ya majadiliano ya kiekumene kwa kukazia umuhimu wa Uekumene wa sala.

Uwepo na ushiriki wa ujumbe wa Vatican uliokuwa unaongozwa na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwenye maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea mtume, hapo tarehe 30 Novemba 2016 huko Istanbul, ulipania kuimarisha Uekumene wa sala unaofumbata upendo katika ukweli na ukweli katika upendo katika kutekeleza na kumwilisha utume wa Kanisa la Kristo katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Majadiliano ya kiekumene yanapania pamoja na mambo mengine kuweka msingi wa ushirikiano katika huduma za kijamii, ili kulinda, kutetea na kuendeleza utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi. Changamoto kubwa kwa sasa mbele ya Makanisa ni haki, amani na maridhiano kati ya watu sanjari na utandawazi wa mshikamano unaojikita katika huduma makini, kielelezo cha imani tendaji inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliye hai! Tabia ya ukanimungu na watu kukengeuka kimaadili, kiutu na katika maisha ya kiroho, kunapelekea watu kukosa huruma na upendo katika maisha yao na hivyo kujikuta wakiwa wakavu kama mti mkavu ambao kamwe hauwezi kuchimbwa dawa!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza alipokutana na kuzungumza na Ujumbe wa Vatican kwenye maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume na msimamizi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Anasema, anaungana na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa masuala ya: uhuru wa kuabudu, haki na amani; upendo na mshikamano, Utu na heshima ya binadamu; umoja na udugu kati ya watu kama njia ya kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, lakini zaidi uhuru wa kuabudu na huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanaonekana kuwa ni mzigo na kero kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Uekumene wa sala kwa ajili ya kuombea amani duniani kama ilivyokuwa hivi karibuni mjini Assisi, imekuwa ni fursa kwa viongozi mbali mbali wa kidini kutambua dhamana na wajibu wao wa kusimama kidete kupinga vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini na kiimani; ili kujenga utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Huduma makini kwa jamii ni kielelezo cha dhati kabisa cha uhuru wa kweli ili kupambana fika na baa la njaa, umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Makanisa yanawajibu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani pamoja na kujizatiti kusimamia kanuni maadili na utu wema. Ujumbe kwa familia ya Mungu uliotolewa baada ya Mtaguso mkuu wa Makanisa ya Kiorthodox uliofanyika mwezi Juni, 2016 kwenye Kisiwa cha Creta ulikazia kwa namna ya pekee: ushuhuda wa imani unaomwilishwa katika matendo. Huu ni ushuhuda uliotolewa hata na akina Petro na Andrea mitume wasimamizi wa Kanisa la Roma na Kanisa la Costantinopoli. Wao waliitikia wito wa Kristo na kuacha yote, wakawa ni wavuvi wa watu, wakatangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ari na moyo mkuu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hata leo hii, Kanisa linaalikwa kuwa ni cheche ya upendo unaoleta mageuzi katika maisha ya watu anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza ametumia fursa hii kumtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Francisko anapojiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 tangu alipozaliwa hapo tarehe 17 Desemba 2016. Anamshukuru kwa salam na matashi mema wakati alipokuwa anaadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa la Costantinopoli. Ni Andrea mtume, aliyemsindikiza Petro kwa Yesu, akimwonesha kuwa ni ukamilifu wa Unabii na Sheria za Musa. Neema na baraka ya Mungu iwe ni nguvu yao ili kuendeleza mchakato wa kiekumene na amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.