2016-12-02 14:20:00

Kanuni ya Imani: Roho Mtakatifu


Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Sehemu hii ya Kanuni ya Imani ndicho kiini cha mahubiri yaliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya Kipapa Ijumaa tarehe 2 Desemba 2016 wakati huu wa Kipindi cha Majilio, kama sehemu ya maandalizi ya kuadhimisha Fumbo la Umwilisho.

Mahubiri kwa mwaka  2016 yanayongozwa na kauli mbiu ”Roho Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini”. Tafakari hii imehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko pamoja, viongozi waandamizi kutoka Vatican na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume! Kwa namna ya pekee kabisa, Padre Cantalamessa amegusia kuhusu mwelekeo mpya uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu pamoja na kuendelea kufafanua kuhusu vipengele vya Roho Mtakatifu vilivyoko kwenye Kanuni ya Imani.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ndio waliotaja kuwa Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Roho Mtakatifu. Huu ndio upya wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yaliyoridhiwa na Mtakatifu Yohane XXIII. Kanisa Katoliki linajiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa Chama cha Kitume cha Uamsho wa Roho Mtakatifu, hapo mwakani, yaani 2017, kielelezo makini cha uamsho wa karama za Roho Mtakatifu zinazolijenga na kuliimarisha Kanisa.

Hii ni tafakari ya kina iliyofanywa na Magwiji wa taalimungu kuanzia kwa akina Congar hadi kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Karne XVI tangu maadhimisho ya Mtaguso wa Costantinopoli wa mwaka 381. Mwaka 1982 kukafanyika Kongamano kubwa la Kimataifa kuhusu Roho Mtakatifu Bwana na Mleta Uzima! Huu ukawa ni mwanzo wa Taalimungu ya Kipengele cha III katika Taalilimungu, yaani Roho Mtakatifu. Kanuni ya Imani ya Nicea-Costantinopoli ni tafakari ya mchakato wa tafsiri rasmi wa imani ya Kanisa kwa Mungu aliye hai. Yaani Mungu Baba muumbaji; Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayekatifuza, kulitegemeza na kulielekeza Kanisa katika ukweli wote, yaani Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima ni kipengele kinachofafanua asili ya Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anayetenda kazi zake kwa njia ya: Imani, Neno, Sakramenti na Sala za Kanisa. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini uzima unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anawapatia waamini maisha mapya kwa kufisha matendo ya mwili yanayoleta kifo! Atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana ni imani inayoonesha Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Padre Cantalamessa amekumbushia kwamba, sehemu hii ya Kanuni ya Imani yaani ”Filioque” ndicho chanzo cha mpasuko kati ya Kanisa la Mashariki na Kanisa la Magharibi. Hii ni imani ya Kanisa katika Umungu Mmoja wenye Nafsi tatu. Roho Mtakatifu hata katika kujificha kwake bado anapendwa katika Fumbo zima la Utatu Mtakatifu na kutambulika kwa alama ya: Mwanga, Moto, Upepo, Maji na Njiwa.

Roho Mtakatifu alinena kwa vinywa vya Manabii, akazungumza kwa njia ya Yesu na sasa anaendelea kuzungumza kwa njia ya Kanisa. Roho Mtakatifu amezungumza katika Sheria, Manabii na kwenye Agano Jipya. Akamshuhudia Kristo alipokuwa anabatizwa Mtoni Yordani kwa alama ya Njiwa, akawashukia Mitume kwa alama ya ndimi za moto! Padre Raniero Cantalamessa anasema Sekwensia ya Roho Mtakatifu inabeba utajiri mkubwa wa mahusiano kati ya Roho Mtakatifu na mwamini kama ”Baba wa maskini, mwanga wa nyoyo za watu na faraja kwa watu. Sekwensia ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya kuzima kiu ya mahitaji ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.