2016-12-01 15:31:00

Papa Francisko apokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Rivera


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 1 Desemba 2016 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mheshimiwa Alfredo Vasques Rivera, Balozi mpya wa Guatemala mjini Vatican. Balozi Rivera alizaliwa kunako mwaka 1965 ana mke na watoto wawili. Balozi Rivera alijipatia elimu yake katika masomo ya sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha San Carlos de Guatemala. Akajiendeleza zaidi katika masuala ya kidiplomasia huko Madrid na Rio Branco del Brasile. Akafuzu vyema katika masuala ya haki za wahamiaji na uraia nchini Marekani pamoja na kujiendeleza katika masuala ya sheria Chuo kikuu cha Denver, Colorado, nchini Marekani.

Katika maisha yake kama mtumishi wa umma amewahi kuwa mkuu wa Idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa; Katibu mkuu mwambata Amerika ya Kusini kwenye taasisi ya MAE. Katibu mkuu msaidizi wa masuala ya Umoja wa Mataifa. Katibu mkuu wa kwanza wa UBalozi wa Guatemala nchini Brazil; Mshauri wa Ubalozi wa Guatemala nchini Canada na Marekani. Ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanasheria nchini Guatemala. Amewahi kuwa Jaalim wa sheria za kimataifa, taasisi za kimataifa, nadharia na vitendo katika mchakato wa majadiliano pamoja na masuala ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Kuanzia mwaka 2010 aliteuliwa kuwa ni Balozi wa Guatemala nchini Israeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.