2016-11-30 15:12:00

Onesheni mshikamano na maskini katika mapambano ya UKIMWI


Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa Katekesi yake, Jumatano tarehe 30 Novemba 2016, amewakumbusha waamini kwamba, tarehe Mosi Desemba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi Duniani. Kuna mamillioni ya watu wanaoishi na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi na kwamba, ni nusu yao tu wanaobahatika kupata dawa za kurefusha maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya wagonjwa wa Ukimwi pamoja na waathirika wote pamoja na kuendeleza mshikamano ili hata maskini waweze kupata fursa ya kuchunguzwa magonjwa na hatimaye kupatiwa tiba muafaka. Baba Mtakatifu anawataka watu wote kuwajibika kimaadili ili kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi duniani.

Baba Mtakatifu amesema pia kwamba, kuanzia tarehe 2- 3 Desemba 2016 huko mjini Abu Dhabi kutafanyika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Falme za Kiarabu na Ufaransa kwa kushirikiana na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, ili kujadili na kupembua kwa kina ”Umuhimu wa kulinda na kutunza makumbusho hasa katika maeneo ya vita”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tema hii imekuja kwa wakati muafaka, changamoto ya kulinda utajiri wa kitamaduni kama sehemu ya mchakato wa kuwalinda binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba tukio hili litafungua ukurasa mpya wa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.