2016-11-30 16:01:00

Komrade Fidel Castro alikuwa ni mtetezi na rafiki wa nchi maskini duniani!


Familia ya Mungu nchini Cuba inaendelea kutoa heshima zake za mwisho kwa Rais mstaafu Fidel Castro Ruz aliyefariki dunia hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 90. Ni kiongozi shupavu aliyesimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha heshima ya wananchi wa Cuba baada ya mapinduzi ya Mwaka 1959. Tangu wakati huo, Cuba ikawekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani, vikwazo ambavyo vimedumu kwa muda wa miaka 54 na wachunguzi wa mambo wanasema, walioteseka zaidi ni wananchi wa kawaida. Kutokana na mchango wa diplomasia ya Vatican, kunako mwaka 2014, Serikali ya Rais Barack Obama wa Marekani ikaanza mchakato wa kurejesha tena mahusiano ya kidiplomasia na Cuba!

Komrade Fidel Castro kama wengi walivyozoea kumwita alikuwa ni mfano bora wa kuigwa na nchi nyingi za Kiafrika na Amerika ya Kusini dhidi ya ukoloni na ukoloni mamboleo ingawa baadhi ya wananchi wa Cuba wanamshutumu kwa kuwa ni dikteta aliyekandamiza uhuru na kudumaza mchakato wa maendeleo endelevu ya watu, leo hii Cuba inaogelea katika hali ngumu ya uchumi na maisha katika ujumla wake. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema, si haki kumhukumu Rais Castro, bali historia itamhukumu kwa wakati wake. Ni kiongozi ambaye alipenda kuwaunganisha watu wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba kwa kuzingatia historia na maisha ya familia ya Mungu nchini Cuba, linapenda kutoa salam za rambi rambi na kuungana kwa namna ya pekee na familia ya Rais mstaafu Fidel Castro, wananchi wa Cuba pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuomboleza msiba wa Rais mstaafu Castro. Maaskofu huku wakiongozwa na imani yao katika ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele, wanapenda kuiweka roho ya Marehemu Rais mstaafu Fidel Castro Ruz chini ya uso wa huruma wa Baba wa mbinguni, ili kwa njia ya Yesu Kristo, Bwana wa historia na maisha na uzima aweze kumkirimia usingizi wa amani na mwisho mkamilifu.

Maaskofu wanachukua fursa hii kwa ajili ya kuombea amani, upendo na mshikamano wa kitaifa hasa wakati huu wa maombolezo mazito chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Cobre, Msimamizi na mwombezi wa familia ya Mungu nchini Cuba. Wanawataka wananchi wote wa Cuba kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili umoja, uzalendo na mafao ya wananchi wote wa Cuba kama ilivyokuwa kwa Josè Martì, Baba na muasisi wa Nchi ya Cuba.

Marehemu Rais mstaafu Fidel Castro anatarajiwa kuzikwa rasmi mjini Santiago de Cuba hapo tarehe 4 Desemba 2016 na kuhudhuriwa na umati wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Cuba, viongozi wakuu wa nchi za Amerika ya Kusini na Afrika ambazo pamoja na hali ngumu ya uchumi kutokana na vikwazo vya kiuchumi, ziliweza kunufaika na huduma mbali mbali kutoka Cuba wakati wa vita baridi. Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Tanzania ni kati ya nchi ambazo zilikuwa na uhusiano wa karibu sana na Cuba katika nyanja mbali mbali hususan katika sekta ya afya na elimu. Katika tukio kama hili, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, tayari amekwisha wasili nchini Cuba ili kutoa heshima zake za mwisho kwa Rais Fidel Castro. Rais Jacob Zuma anasema, Rais Fidel Castro aliwasaidia wazalendo wa Afrika ya Kusini kupambana ubaguzi wa rangi bila hata kuchukua kipande cha dhahabu wala almasi kutoka Afrika ya Kusini, akaonesha ushuhuda wa nchi maskini kushikamana ili kutetea utu na heshima yao.

Cuba inamkumbuka Marehemu Fidel Castro kwa kuwawezesha wananchi kupata elimu ya bure kama sehemu ya haki ya msingi. Kwa upande wake, Rais Raul Castro wa Cuba aliyerithi uongozi kutoka kwa kaka yake Fidel Castro ameishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa kuonesha mshikamano na heshima kutokana na kifo cha Rais mstaafu Fidel Castro. Wanamapinduzi wanasema, mapambano baaaado yanaendelea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.