2016-11-29 09:04:00

Mwilisheni sasa neema na baraka za Mwaka wa Huruma ya Mungu!


Wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wa Madagascar wametafakari kwa pamoja Yesu aliye njia, ukweli na uzima (Rej., Yohane 14:6). Wamefanya tafakari hiyo juu ya Yesu kupitia Neno lake, matendo yake, na maisha yake, ambapo kupitia kwayo Huruma ya Mungu isiyo na mipaka inafunuliwa, huruma ambayo ni chemchemi ya uzima wa kweli. Pamoja na hayo, watu wa Madagascar wana majeraha makubwa na yenye maumivu makali kutokana na kutokuwepo utendaji wa haki na kweli. Hii ni sehemu ya ujumbe kwa waamini, kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar, baada ya mkutano wao mkuu, uliofanyika hivi karibuni, mjini Antananarivo.

Maaskofu Katoliki nchini Madagascar, wamekumbushia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko anayefundisha kwamba, lengo la kuadhimisha Mwaka mtakatifu wa Huruma ya Mungu, ni kuleta uponyaji wa mejeraha yote ya binadamu, na mateso makali ya wana wa Mungu. Maaskofu Katoliki Madagascar wanapomshukuru Mungu kwa kuhitimisha mwaka mtakatifu wa Huruma ya Mungu, wanawaalika waamini wote kuendelea kufungua mioyo yao na kuvumbua kwamba wanaitwa kuishi maisha yao ya kikristu kifua mbele, wakitambua kwamba hakuna malipo zaidi ya uponyaji unaotokana na Kristu, ambaye ndiye kinara wa huruma ya Mungu, jana, leo na hata milele (Rej., Waebrania 13, 8)

Waamini wamwilishe matunda ya neema walizochota wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Neema walizozichota kutoka kwenye maadhimisho ya Sakramenti, katika hija kwenye maeneo matakatifu na kupita mlango mtakatifu, na kwa matendo ya huruma ya kiroho na kimwili. Haya yote wayadumishe maishani mwao, na kamwe wasiyafungie milango. Hayo watayafanikisha iwapo watadumu kwenye muungano na hekima ya kimungu. Tabia njema ambazo zimeonekana katika juhudi za waamini, tayari ni mafao ya pamoja ambayo waamini wa Madagascar wanaweza kuyashirikisha kwa dunia. Jitihada za kutetea haki ni mwaliko kwa kila mwanadamu, zaidi kwa wakristu ambao Kristo kawaonjesha pendo lake, na wanapaswa kulishuhudia pendo hilo kati ya watu.

Ingawa Jubilei ya Huruma ya Mungu imefikia kilele, maisha ya waamini yanaendelea kumshuhudia Kristu, aliye kinara wa Huruma ya Mungu. Hili lizame kwa namna ya pekee katika familia, ambazo ni mahali hakika pa kushirikishana hekima ya Mungu. Hekima ambayo ni chemchemi ya ukweli na rutuba kwa uzima wa mwanadamu. Familia inayoishi imani, na kushirikishana hekima na ukarimu wa Mungu, kwa elimu na malezi bora kwa watoto, ni familia inayoandaa vema kizazi kijacho na maisha bora ya siku za usoni.

Kwa mwaka mpya wa masomo, Maaskofu Katoliki wa Madagascar, wanaalika kila mmoja kujikita katika kuelimisha na kulea vijana katika haki, kweli na hekima ya kimungu. Katika hilo ndipo watakuwa na uhuru wa kweli nchini humo. Wamewaalika watu wa Madagascar kuipenda kweli ili waweze kujikomboa kutokana na dhuluma za aina mbalimbali na mahangaiko kadhaa waliyo nayo. Madagascar inaadhimisha miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia na Vatican, mahusiano ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Madagascar. Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar linawaalika waamini na wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuombea maisha ya amani, furaha na utulivu nchini humo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.