2016-11-29 14:12:00

Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales watahadharisha juu ya athari za Brexit


Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, uamuzi wa Uingereza kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya, yaani Brexit, na Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa la mwaka 2018, zimekuwa mada kuu zilizozungumziwa kwenye mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, waliokutana hivi karibuni mjini Leeds.

Maaskofu hao wameombea amani duniani, kwa namna ya pekee kwa nchi za Sudan kusini, Ukrain na Mashariki ya kati. Kwa upande mwingine wamekemea tabia ya vyombo vya habari kuwaelezea wakimbizi na wahamiaji kana kwamba ni tatizo, badala ya kuwatambua kuwa ni binadamu wenye historia yao na wanaohitaji msaada mkubwa. Kwa upande wao maaskofu wameeleza kwamba uwepo wa wahamiaji katika nchi za Uingereza na Wales ni wa muhimu na fursa kwa jumuiya ya wakatoliki, sababu ni ishara ya utofauti lakini pia mshikamano wa Kanisa Katoliki. Katika baadhi ya parokia kuna watu wa kabila zaidi ya 50, na kwenye mji mkuu kuna takribani ya jumuiya 60 za makabila au vikundi vya mataifa mengine, zenye walezi mapadri.

Maaskofu hawapendezwi hata kidogo na tabia ya kuwabagua na kuwatenga wahamiaji. Kwa mwendo huo huo, maaskofu wa Uingereza na Wales wametahadharisha kuwa kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya, Brexit, iliyotokana na hofu ya myumbo wa uchumi, isiwe chachu ya kupandikiza ubaguzi dhidi ya wahamiaji na wageni. Pamoja na utaratibu wa kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya, Maaskofu Katoliki Uingereza na walles wameweka dhahiri kwamba, wao watabaki kwenye umoja na ushirikiano na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya (CCEE), pamoja na Kamati ya Maaskofu Barani Ulaya (COMECE).  Maaskofu wameonesha kuhofia mahangaiko watakayopata maskini na wanyonge zaidi kutokana na uamuzi wa Uingereza kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatfu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kumekuwepo na matunda mengi sana ya baraka na neema ambayo waamini wamefaidika nayo, na kutoa ushuhuda hata kwa wale wasio wakatoliki. Kwa namna ya pekee, kumekuwepo na ushiriki mkubwa kwenye maadhimisho ya Sakramenti, hasa Sakramenti ya Upatanisho ambapo wengi wamevumbua tena umuhimu, thamani na faida zake kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, ilikuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Kati ya mikakati ya kichungaji iliyowekwa na jimbo la Salford, ilikuwa ni bus lililokuwa na mapadri waungamishi 3. Bus hilo lilizunguka katika miji ya Uingereza ya kaskazini, na zaidi ya waamini 10,000 walipanda bus hilo kwa ajili ya kuungama au kwa ajili ya ushauri wa kiroho. Hii imeamsha sana maisha ya kiroho ya watu wa maeneo hayo.

Kila askofu katika jimbo lake alitembelea magereza na kuonana na wafungwa, ikiwa pia ni mwitikio wa wito wa Baba Mtakatifu Francisko kuchukulia mlango wa magereza kana kwamba ni mlango mtakatifu, ili wafungwa pia wapate kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Baraza la Maaskofu Katoliki la Uingereza na Wales, limeadhimia kuadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa, mwezi Septemba 2018, ambalo litakuwa la pili baada ya lile la mwaka 2005 lililofanyika mjini Birmingham.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.