2016-11-29 10:14:00

Kanuni bora za mawasiliano kadiri ya Papa Francisko!


Alessandro Gisotti, mwandishi wa habari wa Radio Vatican amechapisha kitabu kinachopembua kanuni kumi za mawasiliano bora mintarafu mwelekeo wa Baba Mtakatifu Francisko, kitabu ambacho kitaanza  kuuzwa kwenye maduka ya vitabu kuanzia sasa. Mawasiliano ya jamii yanapaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana na wala si kuta zinazowatenganisha watu! Wala kinzani na migawanyiko inayodhalilisha utu, heshima na mafungamano ya kijamii.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa ndiye aliyeandika utangulizi wa kitabu hiki. Fedha yote itakayopatikana itatumika kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo endelevu inayotekelezwa na Wasalesiani wa Don Bosco. Baba Mtakatifu amekuwa ni kielelezo cha ushuhuda na chombo cha kukutana na watu katika maisha na utume wake, hata wale ambao kutokana na magonjwa na hali zao za maisha wanajikuta wametengwa na jamii, kama ilivyokuwa ugonjwa wa Ukoma kwenye Agano la Kale.

Kwa kukutana na kuwakumbatia watu waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii, Baba Mtakatifu anawarejeshea utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu pale Msalabani. Baba Mtakatifu anafundisha kwa njia ya mfano wa ushuhuda wa maisha yake jinsi ya kuwasiliana na kuhusiana na jirani. Kardinali Tagle anasema, kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati wa mawasiliano unaofumbata mawasiliano ya kweli kati ya binadamu na Muumba wake na kati ya mtu na jirani zake.

Mitandao ya kijamii haina budi kusaidia kuimarisha mchakato wa mawasiliano, umoja, upendo na mshikamano kati ya Mungu na binadamu na kati ya watu ndani ya jamii. Ni mwaliko wa kuwasiliana na wote pasi ya kujenga kuta za utengano kama alivyofanya wakati alipokutana na na Waziri mkuu wa Israeli Bwana Shimon Perez na Abu Mazen kwenye bustani za Vatican au pale Baba Mtakatifu anapowatwangia simu wafungwa magerezani au watu wanaoogelea katika upweke na hali ya kukata tamaa katika maisha! Mawasiliano ya Baba Mtakatifu katika mwelekeo huu yanapania kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kwa kujikita katika matumaini.

Kardinali Tagle anakaza kusema, kiini cha mawasiliani ya binadamu ni utu, heshima na mafao ya wengi; mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Ni mawasiliano yanayolenga kugusa, kuponya na kumrejeshea mtu hadhi yake kama binadamu licha ya mapungufu na udhaifu wake wa kibinadamu. Ni mawasiliano yanayopania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho katika ukweli na uwazi pasi na unafiki! Baba Mtakatifu ni mtu ambaye hapendi unafiki na maisha ya ndumila kuwili!

Baba Mtakatifu Francisko si mtaalam sana wa lugha, lakini ni kiongozi ambaye amebarikiwa kuwasiliana na watu hata katika matendo, ili kuwaonjesha ukaribu, furaha, huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kimsingi, mawasiliano bora yanawawezesha wadau kuwa kama Wasamaria wema wanaothubutu kujitaabisha kwa ajili ya kuwahudumia ndugu zao kwa hali na mali bila ya kujibakiza, changamoto endelevu kama sehemu ya kumwilisha matunda, baraka na neema za maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Wadau wa tasnia ya habari wanapotekeleza dhamana na wajibu wao wanapaswa kwanza kabisa kutanguliza utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi. Hii ndiyo nguvu ya mawasiliano ya jamii inayoweza kutekelezwa kikamilifu na vyombo vya mawasiliano ya jamii anasema Baba Mtakatifu Francisko! Kabla ya jambo lolote lile, kipaumbele cha kwanza ni utu na heshima ya binadamu!  Haya ni mawasiliano yanayopaswa pia kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kila siku na wala si kwa ajili ya wadau wa tasnia ya habari peke yao!

Injili ya familia inaboreshwa kwa maneno ya kawaida kabisa: Tafadhali, Samahani na Asante asali wa moyo wangu! Haya ni maneno ya kawaida lakini yanajenga ukaribu kati ya watu, badala ya kuoneshana na kupimana nguvu na ubabe, utadhani kwamba, familia imegeuka kuwa ni uwanja wa masumbwi! Kanuni za mawasiliano bora ni kitabu kinacholeta chachu ya kukuza na kudumisha mawasiliano bora zaidi ili kusimama kidete kulinda utu na heshima ya binadamu kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, tayari kuendeleza mchakato wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.