2016-11-28 10:18:00

Nchini Australia 2018 ni Mwaka wa Vijana


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Furaha ya Injili anasema kwamba Uinjilishaji wa kweli katika ulimwengu mamboleo unajikita kwa namna ya pekee kabisa katika ushuhuda wa imani tendaji unaomtangaza Kristo Yesu kuwa kweli ni Bwana na Mwalimu. Hii ndiyo Furaha ya Injili inayopaswa kumwilishwa katika maisha ya vijana wa kizazi kipya wanaokabiliana na changamoto nyingi za maisha katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Watu wa Mungu kwa nyakati zote wanapaswa kutangaziwa kwamba, Kristo aliteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua changamoto za maisha ya ndoa na familia aliliwezesha Kanisa kuadhimisha Sinodi mbili za Maaskofu na matunda ya maadhimisho haya ni Wosia wa Kitume “Furaha ya Upendo ndani ya Familia” Amoris Laetitia!

Kama sehemu ya mwendelezo wa tafakari hii ya kina katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Sinodi ya Maaskofu kwa Mwezi Oktoba, Mwaka 2018 ijikite ili kuangalia kwa njia bora zaidi ya kufundisha na kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuwasaidia kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha yao ya ujana, kwani waswahili wanasema, ujana mali, lakini fainali uzeeni! Hapa ni patashika nguo kuchanika! Kanisa linapenda kuwasaidia vijana kufurahia maisha ya ujana sanjari na kukabiliana na changamoto za maisha ya ujana kwa ari na moyo mkuu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia kunako mwaka 2018 linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 10 tangu Kanisa lilipoadhimisha Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2008, kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya maadhimisho haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limeamua kwamba, mwaka 2018 uwe ni Mwaka wa Vijana Kitaifa nchini Australia. Mwaka huu utazinduliwa rasmi tarehe 29 Novemba 2016.

Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa vijana kwa kutambua kwmba, vijana ni jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Hii ni fursa ya kuendeleza ari na moyo uliojitokeza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2008. Vijana ambao ni tumaini la Kanisa la taifa wanapaswa kujengewa uwezo wa kujishikamanisha na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku: kwa kumsikiliza katika Neno; katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, katika maisha adili na sala.

Vijana wahamasishwa kushirikisha karama, vipaji, matumaini na mahangaiko yao katika Jumuiya ya waamini na Jamii inayowazunguka, ili kusaidiana mintarafu mwanga wa Injili ya matumaini. Maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Kitaifa nchini Australia yatajikita kwa namna ya pekee katika Jumuiya za waamini, ili ziweze kuwasaidia vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa vijana wenzao wanaokosa dira na mwelekeo wa maisha kutokana na changamoto mbali mbali za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.