2016-11-25 15:30:00

Utajiri wa Kipindi cha Majilio


Kipindi cha majilio huanza kati ya Novemba 27 na Desemba 3 na kumalizika kabla ya masifu ya jioni ya mkesha wa Noeli.  Katika Jumapili na siku za wiki utukufu haisemwi. Jumapili zote haziingiliwi na Liturujia nyingine yo yote na ikiwapo liturjia nyingine basi hufanyika Jumamosi kabla ya kuanza kipindi cha majilio. Jumapili kati ya Desemba 17 hadi 24  zasisitiza zaidi ujio wa Bwana na maandalizi ya Sherehe ya Noeli, Neno wa Mungu anapofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake kama kielelezo makini cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Mungu anayetembea katika maisha na historia ya watu wake!

Kipindi cha majilio ni kipindi cha mwaka wa Kanisa chenye kumbukumbu za maisha, kifo, na ufufuko wa Bwana. Ni kumbukumbu ya mafumbo, matendo ya Kristo, lakini siyo kumbukumbu ya kitu kilicho mbali, cha zamani kilichopita - ni kipindi cha neema na umaana wa alichofanya Yesu. Hutukumbusha kuwa jambo hilo lipo kati yetu. Tunasherehekea sikukuu za mwaka wa Liturujia - ndiyo mwanzo wa imani yetu. Sisi tunakua ili kuenenda na Kristo na tunaishi katika Fumbo hili la Sakramenti. Majilio ni kipindi cha majuma manne (4) na kipindi hiki huhitimishwa na sikukuu ya Noeli. Katika kipindi hiki:

Kipindi hiki:

Yesu pia ni hakimu na hiyvo majilio yatukumbusha hali hiyo, uwepo wetu kama mahujaji - tuko safarini, tusibanwe na mambo ya dunia. Hutualika tena kutambua na kuishi uwepo wa Mungu kati yetu. Liturujia inatuangalisha hivyo:

Ili ajapo Bwana - atukute tu macho, tukiwa na taa zetu mikononi na zikiwaka na kuwa na mioyo iliyo tayari kumpokea mfalme wa Mbingu na dunia. Hiki ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini. Tunakumbuka nini? Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu - tunatafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu akaupa umaana uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu, akatuonesha maana ya maisha ya Kimungu - eti Mungu akawa mwanadamu. Tumshukuru Mungu kwa Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake, ufunuo wa huruma ya Baba wa milele! Tunatumaini nini? Tunatumaini ujio mtakatifu aliotuahidia, jumuiya takatifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu. Angalia Pope Benedict XVI (Joseph Card Ratzinger) “seek that what is above” 1986 ….. Memory Awakanes Hope.

Kumbukumbu zinaamsha matumaini. Tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu, akakaa nasi na tunahusisha matumaini yetu kwamba Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Katika kipindi cha majilio tunakumbuka matendo makuu ya Mungu na tunatumainia upendo mkuu wa Mungu. Mt. Ireneo katika maandishi yake karne ya 3 “DHIDI YA UZUSHI” “AGAINST HERESIES” anaandika hivi: akielezea kazi ya Kristo; anasema, imani ya Kikristo inatambua kuwa Mungu ni mmoja na Yesu Kristo mwanae, Bwana wetu, ambaye vitu vyote viko chini yake. Kati ya vitu hivyo yupo mwanadamu, ambaye ni sura na mfano wake Mungu. Hivyo naye mwanadamu ni mali yake, naye Mungu asiyeonekana, akaonekana kwetu, tukamfahamu, “3,16,6 Gia’ e Ancora” (Already and not Yet) CCCXX, 1979, p 268.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.