2016-11-24 09:51:00

Utunzaji bora wa vyanzo vya maji ni muhimu kwa amani na usalama wa dunia!


Upungufu wa maji duniani unaendelea kuwa tishio kwa maisha bora ya mwanadamu na mazingira yake. Wakati maji yanachukua theluthi mbili ya sakafu ya dunia, bado upatikanaji wa maji safi na salama unapungua siku hadi siku. Sauti ya Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa kimataifa, imesikika alipokuwa akichangia hoja ya mdahalo huru kuhusu maji, usalama na amani kimataifa, siku ya Jumanne tarehe 22 Novemba 2016, Jijini New York.

Kupanuka kwa majangwa, uharibifu wa misitu, na ongezeko la ukame vinaamsha maswali mengi juu ya janga la kukosekana kwa maji safi na salama kwa siku za usoni. Baadhi ya sehemu duniani zimekuwa na ukosefu wa maji sababu ya mahali sehemu hizo zilipo kijiografia. Jambo linalosikitisha leo ni ukweli dhahiri kuwa, hata maeneo ambayo yamebahatika kuwa na nishati ya maji, nishati hiyo imeanza kuwa adimu ama sio salama kutokana na uchafuzi wa mazingira na uharibifu unaofanywa na mwanadamu mwenyewe, sauti ya Askofu mkuu Auza imesikika ikikosoa kutokujali huko kwa baadhi ya watu.

Mabadiliko ya tabianchi, shughuli za uchimbaji ovyo wa madini, kilimo na uzalishaji viwandani katika sehemu nyingi hasa katika nchi maskini zaidi duniani pasipo na utaratibu na udhibiti makini wa masuala hayo, nishati ya maji inachafuliwa sana kiasi cha kuhatarisha afya ya binadamu. Uhitaji wa maji leo ni mkubwa zaidi kuliko upatikanaji wake. Upungufu wa nishati hii unaathiri zaidi nchi za Afrika ambapo kutokana na uchafuzi wa mazingira, maji safi na salama hayapatikani kiurahisi, lakini pia ukame unaopelekea kukosekana kwa mazao. 

Iwapo hatua makini na za haraka hazitachukuliwa, tatizo la maji duniani linaweza kuwa ndio vita ya tatu ya dunia. Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea ofisi za Shirika la Kilimo na Chakula la kimataifa (FAO), alitahadharisha akisema: nishati ya maji haipatikani bure bure kama inavyofikirika kila wakati. Ni tatizo kubwa linaloweza kupelekea watu kutumbukia kwenye vita. Maji ni ya lazima kwa afya na hali bora ya maisha ya mwanadamu. Jambo la kusikitisha ni kuona jinsi maji yasio safi na salama yanavyokuwa chanzo cha vifo vya watu wengi, hasa watoto, kutokana na magonjwa kama kipindupindu. Kumekuwa na tabia kwa karne ya leo kujimilikisha nishati ya maji kwa baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji. Nishati ya maji ni haki ya kila mwanadamu, iwapo itaanza kudhaniwa kuwa ni miliki ya wachache, deni la kuwahudumia maskini na kuwahakikishia haki zao msingi litazidi kukua. Utekelezaji na utetezi wa haki za binadamu uzingatie pia nishati ya maji kama hitaji na haki msingi.

Askofu mkuu Auza, amesisitiza kusema kwamba, ujumbe wake katika Umoja wa Mataifa unaamini kuwa mbinu za kisasa za maendeleo ya sayansi na teknolojia zinaweza kutumiwa katika uzalishaji bila kutumia maji mengi sana ikawa ni kufuru na kunyima wengine haki msingi ya maji, na pia mbinu hizo za kisasa zaweza kutumika kuepuka uzalishaji wa viwandani unaochafua mazingira na kuhatarisha maji safi na salama. Hayo yatatendeka kwa kuzingatia na kuthamini pia suluhu za jamii asilia katika kutengeneza na kutunza mfumo mzuri wa maji katika maeneo yao.

Mwishoni, sauti ya Askofu mkuu Bernadirto Auza katika mdahalo huru wa usalama kwenye Umoja wa Mataifa, imewaalika wajumbe kuzingatia umuhimu wa elimu katika kuwaelewesha watu thamani ya nishati msingi ya maji. Elimu itolewe kuhusu utunzaji, matumizi mazuri, na mgawanyo wa uwiano wa nishati hii kwa ajili ya mafao ya wote. Vinginevyo changamoto ya maji safi na salama itabaki kuwa hatari kwa nyanja zote za uchumi, afya, teknolojia, siasa, jamii na hata maadili.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.