2016-11-24 15:00:00

Kumbu kumbu ya Bikira Maria Mama Yetu wa Guadalupe!


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 12 Desemba 2016 wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Guadalupe, ataungana na mamillioni ya familia ya Mungu kutoka Amerika ya Kusini kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya heshima ya Bikira Maria Mama yetu wa Guadalupe. Ibada hii inatarajiwa kuanza saa 12:00 jioni kwa saa za Ulaya, lakini itatanguliwa kwa Ibada ya Rozari takatifu, muhtasari wa huruma ya Mungu katika historia ya wokovu! Waamini na wanadiplomasia kutoka katika nchi za Amerika ya Kusini wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican wanatarajiwa kushiriki kwa wingi.

Tume ya Kipapa kwa Amerika ya Kusini inakumbusha kwamba, kwa mara ya kwanza kumbu kumbu hii iliadhimishwa mjini Vatican tarehe 12 Desemba 2011 na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kama kumbu kumbu ya Jubilei ya uhuru kwa nchi nyingi za Amerika ya Kusini. Kunako mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko akaonesha nia njema ya kutaka kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, kama kumbu kumbu ya tukio hili miaka 50 iliyopita wakati Mwenyeheri Paulo VI alipoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kuongozwa na nyimbo kutoka kwa wenyeji.

Baba Mtakatifu Francisko akabahatika kutembelea Mexico kuanzia tarehe 12- 18 Februari 2016 pamoja na kutoa heshima zake kwa Bikira Maria, Mama Yetu wa Guadalupe. Mwaka huu, maadhimisho haya ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa wenyeheri kutoka Amerika ya Kusini waliotangazwa hivi karibuni na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu. Hawa ni Padre Josè Gabriel del Rosario pamoja na Josè Sànchez del Rio. Nyimbo za Ibada ya Misa takatifu zitakuwa ni zile zilizotungwa enzi hizo kwa heshima ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Guadalupe na Mtakatifu Juan Diego.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.