2016-11-23 08:32:00

Njia za huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume ”Misericordia et misera” yaani ”Huruma na amani” anapenda kuwashukuru Wamissionari wa huruma ya Mungu ambao waliotumwa sehemu mbali mbali za dunia kama ishara ya hamasa ya kimama ya Kanisa kwa Taifa la Mungu, kwa kuwawezesha waamini kuonja utajiri wa huruma ya Mungu unaofumbatwa katika fumbo la imani.

Wamissionari hawa wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, iliyowawezesha waamini kuonja tenda ndani mwao furaha ya imani kwa kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu ni kwa waamini kuendelea kujipatanisha na Mungu kama sehemu ya hija ya maisha yao hapa duniani pamoja na kuendelea kugundua nguvu ya upendo wa Mungu inayowawezesha waamini kuwa tena viumbe wapya!

Baba Mtakatifu anawapongeza kwa huduma hii njema ya shughuli za kichungaji iliyowawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa msamaha wakati wote wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anaendelea kukaza akisema, huduma hii inaendelea hata baada ya kufungwa rasmi kwa malango ya huruma ya Mungu na itakuwa inaratibiwa na Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya, kielelezo cha uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika huduma hii nyeti!

Itakumbukwa kwamba, Padre Wojciech Adam Koscielniak, kutoka Kituo cha Hija cha Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, ni kati ya Wamissionari wa huruma ya Mungu waliotumwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waamini waliokuwa wanatubu na kumwongokea Mungu ili kushinda vikwazo, tayari kuanza maisha mapya yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapembua kwa kina mapana njia tatu za huruma ya Mungu yaani: Ombeni huruma yake, Iweni na huruma, Mtumainieni kabisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.