2016-11-23 14:28:00

Kambi tatu za wakimbizi zafurika nchini Tanzania


Katika Jamhuri ya muungano wa Tanzania, muda sio mrefu kunaelekea kulipuka tatizo kubwa la kufurika kwa wakimbizi. Kwa miezi 4 iliyopita, kumekuwa na ongezeko kubwa la wakimbizi kutoka Burundi, wakati huo mamia ya maelfu ya wakimbizi katika kambi tatu nchini Tanzania wanaishi katika hali ngumu na zenye changamoto nyingi.

Tayari mpaka sasa kambi hizo zina jumla ya takribani wakimbizi 250,000 kutoka Burundi na Congo, na kumekuwa na majadiliano kuona uwezekano wa kufungua kambi ya nne. Karibu kila mwezi Tanzania inapokea wakimbizi 10,000 kutoka Burundi, wakati kwa mwezi Oktoba mwaka huu, wameingia wakimbizi 850 kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Congo.

Taarifa hizi zimetolewa na Shirika la Madaktari wasio na mipaka. David Nash, mkuu wa huduma za shirika hilo katika Afrika mashariki amesema, wanatarajia kufikia mwisho wa mwaka huu 2016, idadi ya wakimbizi katika kambi hizo itavuka 280,000. Hali hii, itakuwa moja ya matatizo makubwa kwa bara la Afrika.

Hali ilianza kuwa ngumu mnamo mwezi Mei 2015, ambapo katika kambi ya Nyarugusu walipokelewa wakimbizi 60,000 kutokea Congo. Kufuatia kufurika kwa wakimbizi kwa muda mfupi, serikali ya Tanzania ililazimika kufungua kambi zingine mbili. Mwezi Oktoba mwaka jana 2015 ikafunguliwa kambi ya wakimbizi Nduta, na mwezi Januari mwaka huu 2016 ikafunguliwa kambi ya Mtendeli. Kwa vyovyote vile, kwa sasa kuna hitaji la kambi ya nne, ambayo bado haijaamuliwa kufunguliwa maeneo yapi.

Hali za wakimbizi sio nzuri hasa kwa upande wa afya. Wingi wa wakimbizi kiasi hicho katika kambi, kunaleta ugumu wa kuwa na mazingira safi ya kujipatia haja msingi. Kwa sababu hiyo, wakimbizi wamo kwenye hatari kubwa ya maambukizi ya magonjwa kama maleria, kipindupindu na magonjwa mengine ambukizi.

Serikali ya Tanzania itahitaji kuungwa mkono zaidi na mashirika ya kimataifa na watu wote wenye mapenzi mema, ili kukabiliana na changamoto hiyo, na kufanikisha mazingira mazuri ya kuishi wakimbizi, kupata mahitaji yao msingi, kuishi kwa furaha na uhuru kama binadamu wengine, na kuepuka milipuko ya magonjwa na majanga mengine yanayoweza kuwaathiri wakimbizi na rai wa nchi hiyo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.